NAIBU Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Deogratius Ndejembi ametoa siku saba kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya  John John Nchimbi kuhakikisha kuwa  milango iliyowekwa kwenye ujenzi wa Shule ya Msingi Tonya inabadilishwa ili kuendana na thamani ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi huo.

Ndejembi ametoa agizo hilo kwenye ziara yake ya kukagua shule tatu za msingi zinazotekelezwa kupitia mradi wa BOOST na shule mbili za sekondari zinazotekelezwa kupitia mradi wa maboresho wa SEQUIP jijini humo.

Akiwa shuleni hapo, Mhe.Ndejembi amesema pamoja na kuona mradi wa shule hiyo mpya umekamilika lakini hajaridhishwa na baadhi ya maeneo ikiwemo baadhi ya milango kuanza kupasuka mapema na hivyo kuagiza milango hiyo kubadilishwa haraka ndani ya siku saba.

"Nimefanya ziara kwenye shule tatu za msingi na mbili za sekondari, niwapongeze Jiji la Mbeya kwa kasi kubwa mliyonayo ya kutekeleza miradi hii iliyoletwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, haya mapungufu niliyoyaona niagize yafanyiwe kazi haraka na ndani ya siku saba yawe yamefanyika,”amesema.

Ameagiza kamati zinazosimamia miradi hiyo nchini kuhakikisha mafundi na wazabuni wanaleta vifaa vilivyo na ubora na ujenzi pia unatekelezwa kwa ubora ili kuendana na thamani ya fedha iliyotolewa na serikali.

“Niwaagize pia Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wazabuni na mafundi ambao watashindwa kutekeleza miradi hii kwa ubora uliowekwa basi wachukuliwe hatua na wasiwape tenda nyingine na badala yake muwape kazi wazabuni na mafundi wenye kujali fedha hizi zinazoletwa kwa ajili ya maendeleo," amesema Mhe Ndejembi.

Naye, Mkurugenzi wa Jiji hilo, John Nchimbi amemshukuru Rais Samia kwa fedha nyingi za miradi ya maendeleo zilizoletwa ndani ya Jiji hilo na kuahidi kushughulikia changamoto zilizobainika kwenye ziara ya Naibu Waziri huyo.







Share To:

Post A Comment: