Na John Walter-Manyara

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange amewaonya wananchi dhidi ya kupuuza kudai risiti za kieletroniki (EFD) wanaponunua bidhaa akisema, tabia hiyo inakwamisha jitihada za serikali kukusanya kodi.

Onyo hilo amelitoa wakati akizindua kampeni ya TUWAJIBIKE  kwa ajili kuelimisha wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kutoa na kudai  risiti za EFD baada ya huduma inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato mkoa wa Manyara.

Twange kupitia mazoezi (Jogging) aliungana na wakala wa mapato (TRA) mkoa wa Manyara kubandika stika maalum  kwenye Migahawa mbalimbali mjini Babati zenye ujumbe wa kuwakumbusha wafanyabiashara na wananchi kutoa na kudai ili kuhakikisha serikali inakusanya fedha za kutosha kuhudumia miradi ya maendeleo.

"Nchi inaendeshwa kwa kodi za wananchi hata miradi mbalimbali ya maendeleo mnayoiona inatokana na kodi" alisema Twange

Meneja wa TRA Manyara,David Nyolobi  amesema kampeni hiyo inalenga kuwaelimisha wafanyabiashara na umma kwa ujumla umuhimu wa kulipa kodi na  kwamba hawatasita kumchukulia hatua yeyote atakayekiuka utaratibu huo.

Amesema watafanya operesheni maalum kuwawajibisha wafanyabiashara wasiotoa risiti za kieletroniki pamoja na wananchi wasiodai risiti pindi wanapofanya manunuzi.

Katibu wa TCCIA mkoa wa Manyara Zainabu Rajabu amesema watendelea kuwakumbusha wafanyabiashara umuhimu wa kutoa risiti wanapotoa huduma.

Share To:

Post A Comment: