Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akikagua mabanda kabla ya kufungua mkutano wa nne wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi (AQRB) wakimsikiliza naibu waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya (Hayupo Pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa bodi hiyo, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey kasekenya (wa nne waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na wakadiriaji majenzi (AQRB) jijini Dodoma. |
Na,Okuly Julius - Dodoma
Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), wametakiwa kuwachukulia hatua wataalamu wote waliosajiliwa na Bodi hiyo ambao wanakwenda kinyume na taaluma hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya wakati akifungua Mkutano wa 4 wa AQRB,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa.
"Kuna wataalamu mmewasajili ila wengine kwa makusudi wanakiuka utaratibu waliowekewa na Bodi yenu ya kitaaluma hao msiwavumilie wafuatilieni na washughulikieni wasije wakawachafulia kazi nzuri mnayoifanya,"amesema Kasekenya
Mha.Kasekenya amesema ni vyema wataalamu hao wa kusanifu Majengo na kukadiria Majenzi waungane na kutengeneza nguvu ya pamoja ili waweze kupata mikataba ya Miradi Mikubwa na kuisaidia Serikali kuokoa gharama za kutafuta wataalamu kutoka nje ya nchi.
"Tambueni taifa linafahamu mchango wenu na linathamini wataalamu wa ndani na ndio maana Mhe.Bashungwa kama Waziri mwenye Dhamana ya Wizara hii anawashauri muunganishe nguvu ili muweze kupata tenda kubwa hapa Nchini na nchi itapunguza gharama ya kuwatoa wataalamu kutoka nje ya nchi," amesema Kasekenya
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo, amesema Wizara itaendelea kutoa ufadhili wa mafunzo kwa vitendo kwa wataalamu wa Taaluma za wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi nchini.
Pia amesema kuwa, Bodi itaanzisha mfuko wa maendeleo ya wanafunzi ili kuweza kutenga fedha za kusaidia vijana wenye taalamu za ubunifu majengo na wakadiriaji majenzi.
“Nimeambiwa katika mwaka huu wa fedha 2023/24 Wizara ya Ujenzi imetenga kiasi cha shilingi milioni 748 kwenye bajeti yake kwa ajili ya mpango wa mafunzo wa EAPP, nia ni kuongeza idadi ya wahitimu wanaopata mafunzo hayo”, amesema Mhandisi Kasekenya
Aidha, amezielekeza Bodi za AQRB, ERB, CRB na NCC ziweze kufanya kazi kwa ukaribu na kushirikiana ili kuhakikisha kuwa Taifa linafaidika na huduma za kitaalamu zinazotolewa na wataalamu na makampuni yaliyosajiliwa na Bodi hizo.
Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi, Arch. Edwin Nnunduma amesema kuwa wanampango wa kusajili wataalamu 5000 kufikia mwaka 2026, katika kada za kati.
“Serikali kupitia Bodi hii tumejipanga kukagua miradi zaidi ya 3014 kwa Taasisi binafsi na Serikali kwa ujumla, pia ameongeza kuwa juhudi zinaendelea kuweza kusajili wataalam pamoja na Makampuni.” amesema Arch. Nnunduma
Halikadhalika, Arch. Nnnunduma amesema kuwa ili kuboresha utendaji na ufanisi wa wafanyakazi, Bodi inatarajia kuanzisha mfumo wa kieletroniki kwa watumishi wote.
Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji majenzi (AQRB) inaendelea na Mkutano wake wa 4 kwa siku mbili jijini Dodoma.
Post A Comment: