Imeelezwa kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wenye Viwanda, Wafanyabiashara na Wawekezaji kushiriki katika ukuzaji wa uchumi hususan kwenye Sekta ya Viwanda.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango kwenye Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ufunguzi wa Mtambo Mpya wa Mabati ya Rangi kampuni ya ALAF jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa, tukio hilo ni sehemu ya matunda ya juhudi kubwa zinazofanywa na Uongozi wa Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji na pia kwa maono yake ya kuiamini Sekta Binafsi katika kujenga uchumi imara wa nchi.
“Napenda kuwaahidi kwamba, wenye viwanda, wafanyabiashara na wawekezaji, Serikali itawapa ushirikiano. Kwa upande wenu, mnao wajibu wa kuzingatia uendelevu wa ubora na tija kulingana na viwango vinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa katika shughuli za uzalishaji hatimae kunufaika zaidi na fursa za masoko zilizopo na zinazoendelea kujitokeza,’’ ameeleza Dkt. Biteko
Aidha, Dkt. Biteko amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa ALAF Limited, Bw. Ashish Mistry, Bodi na Menejimenti ya kiwanda cha ALAF kwa kuamua kujenga mtambo huo wa kwanza nchini na wa kisasa utakaotumika kutengeneza mabati ya rangi nchini.
“Nimeelezwa kwamba mtambo huu umegharimu jumla ya Dola za Marekani milioni 25 na unatarajiwa kutoa ajira kwa watu 500. Ni dhahiri kuwa kukamilika kwake kunatoa mwelekeo mpya kwa Taifa letu kwa kuwa imekuwa ni ndoto ya nchi nyingi za Afrika kuwa na kiwanda kama hiki,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, amesema kuzinduliwa kwa mtambo huo kunatoa fursa mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huo ikiwemo nafasi za ajira zitakazotolewa na kiwanda hicho kwa Watanzania.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Athuman Angenya amesema kuwa kiwanda hicho kimeendelea kutengeneza bidhaa zenye ubora nchini jambo linalofanya wafanye vizuri katika soko.
Vile vile, Mwenyekiti wa Bodi kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt. Bilinith Mahenge amesema kuwa kituo hicho kimeendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi.
Pamoja na washiriki wengine, hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa SAFAL Group, Bw. Anders Lindgren, Wakuu wa Wilaya wa Jiji la Dar es salaam, wadau na wafanyakazi kutoka ALAF.
Post A Comment: