Na Said Mwishehe


WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amesema Wizara hiyo imeendelea na mikakati mbalimbali ya kutekeleza maono ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha vijana wengi na wanawake wanajihusisha na sekta ya mifugo na uvuvi.

Amesema katika kutekeleza maono hayo tayari Wizara hiyo imeanza Mradi wa BBT ambapo vijana 200 wameanza kupewa elimu ya kununua mifugo na kuinenesha na kisha kuiuza na wengine wakiendelea na unenepeshaji wa jongo na Kaa.

Waziri Ulega ameyasema hayo leo Septemba 3, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Wahariri na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu ambao pia ulihusisha mawaziri wanaotoka katika wizara za kilimo na uvuvi.

Lengo la Mkutano huo ni kuzungumzia namna ambavyo Tanzania imejipanga kuelekea Mkutano wa Jukwaa la Chakula Afrika ambapo viongozi wakuu wa nchi za Afrika na wadau wa chakula zaidi ya 3000 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo.

Akizungumza mbele ya Wahariri,  Waziri Ulega ametumia nafasi hiyo kuelezea mambo muhimu ambayo wanaendelea kuyatekeleza kupitia Wizara yake lakini kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo inayosimamiwa na Waziri Hussein Bashe.

Waziri Ulega alianza kueleze umuhimu wa Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chalula Afrika ambao utafanyika nchini kuanzia Septemba 5 hadi Septemba 8 mwaka huu ambapo amesisitiza mkutano utatoa fursa pia kwenye sekta ya mifugo na uvuvi.

"Tumshukuru Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan  kwa jitihada zake ambazo zimefanya mkutano huu uje Tanzania.Huko mwanzo mkutano ulikuwa wa kilimo tu lakini kwa mara ya kwanza tunaufanya ukiwa umejumuisha mifugo na uvuvi...

" Na hiyo inaonesha nia ya Rais kuwainua wananchi walio wengi kwenye kilimo mazao, kilimo mifugo na kilimo uvuvi. Wenzetu huko ni kitu kimoja huku kwetu tunajitegemea.

"Hivyo hizi sekta zinazogusa wengi kwa maono ya Rais anataka zipewe kipaumbele kwenye masoko na zilete tija na ndio msingi wa mkutano huu na nimejibu vizuri  kwanini umejumuisha mifugo na uvuvi, " amesema Waziri Ulega.

Akifafanua kuhusu masoko ya mifugo na nyama,  amesema nchi yetu imejipanga na kuweka mikakati mbalimbali kuhusu soko la nyama lakini kikubwa ni kuhamasisha kwani   biashara ya mifugo ni fursa adhimu.

"Nitoe ombi kwa ndugu zetu wahariri wa vyombo vya habari mtusaidie kueleze biashara hii kuanzia unenepeshaji, kuiingiza kwenye viwanda na kuchakata.

"Tunafahamu changamoto ni mtaji hivyo tunataka kuzumgumza na benki na taasisi za fedha tuwaaminishe waingize fedha huko,  wafugaji wengi tulionao hawako kwenye biashara hii,  wizarani kitu tunachofanya wafugaji tunawachukua kama wazalishaji wa kwanza.

"Hivyo hatua ya pili itakuwa sisi kuinenepesha  mifugo na kuingiza kwenye soko, hivyo lazi mitaji ipatikane.
Mipango yetu ni pamoja na kutumia ardhi zetu yakiwemo mashamba ya Narco, " amefafanua.

Pia amesema  lengo la Wizara ni kupeleka vijana wengi kupitia mpango wa BBT ambao tayari kwenye wizara hiyo umeshaanza na vijana wanakwenda kwenye midana wanafundishwa namna ya kuchagua ng'ombe na watalaam ndio wanafundisha.

Ameongeza kwa hiyo vijana wameanzia sokoni na wameanza na vijana 240 na kila kijana ana ng'ombe 10 ambao waliwafuata mdani."Wameshauza ng'ombe 900 na wamepata faida milioni 74."

Aidha amesema kwenye uvuvi walianzaa na vijana 200 wapo walioanza na vizimba kule Ziwa Victoria na Ukanda wa Pwani wapo vijana ambao wananenepesha jongoo na Kaa.

"Safari hii tunakwenda na vijana 300 na tukiwa kwenye tamasha la kizimkazi Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo maalum na sisi tumeshafanya mazungumzo na wenzetu Zanzibar.

" Tutakwenda na jambo hili na Zanzibar tutachukua vijana 50 ili waungane na vijana wenzao wa bara.Kwa hiyo BBT katika mifugo na uvuvi tunakwenda vizuri na lengo la Rais ni kuona vijana wengi na wanawake wanahusishwa katika sekta hizi.

"Lengo tunataka kwa mfano vijana wanaolima zao la Zabibu kule Dodoma basi pamoja na Zabibu  tunataka huku nyuma wafanye na ufugaji , wananenepeshe mbuzi, ng'ombe na maziwa, lengo tunataka vijana wawe matajiri.

"Katika hili la unenepeshaji mifugo  nilizungumza bungeni na Mbeya kuhusu kuwa na gest za mifugo na habari ilikuwa kubwa, nikaletewa picha ya ng'ombe akiwa gesti lakini tutaendelea kulieleza hili la unenepeshaji na tutaeleweka."
Share To:

Post A Comment: