Na Immaculate Makilika - MAELEZO
Wananchi wa Wilaya ya Masasi, Mkoa wa Mtwara wamepongeza jitihada za Serikali katika kilimo cha zao la mbaazi ambalo limeendelea kuwanufaisha.
Mkazi wa Wilaya ya Masasi, Kata ya Jida, Bi Fatma Ismail amesema kuwa wamefarijika na ziara ya Mhe. Rais Samia mkoani humo na kuwa wanampongeza kwa jitihada zilizofanywa na Serikali yake katika zao la mbaazi.
"Mbaazi zinauzika kwa bei nzuri na sasa hivi mbaazi ni pesa si mboga tena", anaeleza Bi. Fatma.
Amefafanua "Awali tulikua tunalima mbaza na kuuza kilo moja kwa bei ya shilingi 100 hadi 500, sasa hivi tumeuza mbaazi kilo moja kwa shilingi 2000 hadi 2500 Serikali imetusaidia sana hii bei haijawahi kutokea".
Pia, ameishukuru Serikali kwa kuwapa elimu na fursa mbalimbali ambapo katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane ya mwaka 2023 wamepata fursa ya kupeleka bidhaa zao zikiwa katika makasha na wameuza kwa bei rafiki.
Kwa upande wake, Mkulima wa mazao mchanganyiko, Bw. John Abeid amesema kuwa bei ya mbaazi haikuwa rafiki na soko liliparanganyika.
"Lakini chini ya uongozi wa Mhe. Rais Samia hususan msimu wa mwaka huu wa mbaazi soko limebadilika na wananchi tumefurahi kuhusu bei ambayo hadi sasa si chini ya shilingi 2000, tunampongeza sana na kumshukuru Mhe. Rais na tunaomba aendelee katika zao la korosho ili tupate bei zaidi", ameeleza Bw. Abeid.
Naye, Mkazi wa Wilaya ya Masasi, Mtaa wa Ally Musa, Mlundelunde amesema "Kwenye mbaazi mambo yameenda vizuri ni kweli kuwa hakuna utawala wowote uliowahi kutusaidia kuhusu bei kama sasa. Pia, hata wanunuzi hawakunyanyaswa wakati wa kupima na mbaazi zilikuwa nzuri sana", amesema Bw. Mussa.
Aidha, amesisitiza"Kutokana na wakulima kuuza kwa wingi mbaazi, mbegu zitakuwa chache hivyo tunaomba Serikali itusaidie kutuletea mbegu za mbaazi kwa wingi".
Post A Comment: