Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema atawashughulikia Wakurugenzi Mamlaka za Serikali za Mitaa ambao wamekaa na fedha za miradi muda mrefu bila kuanza utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo leo Septemba 13, 2023 wakati wa kuzungumza na baadhi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mara baada ya kukagua ujenzi wa shule ya Bungu.
Shule ya Bungu imejengwa kupitia fedha za kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa shule za awali na msingi Tanzania (BOOST).
Amesema baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri wamekaa na fedha za miradi muda mrefu bila kuanza utekelezaji wa miradi hiyo hatua inayofanya wananchi wanaendelea kuteseka.
"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wameshatoa fedha za miradi na baadhi ya Wakurugenzi wamekaa nazo bila kuanza kutekeleza na kufanya wananchi waendelee kuteseka katika kipindi changu sitawaelewa nitawashughulikia ipasavyo."
"Mkurugenzi anapokea fedha anakaa kimya, Mwenyekiti wa Halmashauri yake hajui, Mkuu wa Wilaya hajui na Mkuu wa Mkoa naye hajui anayejua ni yeye tu na hafanyi chochote, fedha zimekaa tu kwenye akaunti, sasa ambaye atashindwa kukamilisha miradi hii ndani ya muda uliopangwa sitamfumbia macho."
Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wanapopokea fedha wahakikishe wanawajulisha viongozi wa Mkoa, Wilaya na menejimenti yaki ili kwa pamoja wakubaliane namna bora ya kutekelezwe mradi kwa haraka na kwa ubora.
" Nitarejea maelekezo yangu wakati naripoti kwenye Wizara hii kuwa sitaongeza muda wa utekelezaji wa miradi, kama Halmashauri ilipata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Boost au SEQUIP au afya na hata miundombinu ya barabara sitaongeza muda hata siku moja, ninataka kuona miradi hiyo ikikamilika ndani ya muda."
" Sitakubali kuona mwananchi anataabika kwa kukosa huduma bora wakati fedha iko kwenye akaunti ya Halmashauri na Rais Samia alishatoa fedha hiyo siku nyingi katika hili sitokuelewa. Mkurugenzi yeyote anaye kwamisha utekelezaji wa miradi nitamshughulikia ipasavyo."
Amesema miradi yote ya afya iliyopelekewa fedha inatakiwa kukamilika Oktoba 30 mwaka huu huku ile ya elimu imepangwa kukamilika Septemba 30 mwaka huu.
" Sitaongeza hata siku moja kama hamjakamilisha fanyeni kazi kwa saa 24 ili iweze kukamilika ndani ya muda uliotolewa’ alisisitiza Mhe. Mchengerwa.
Post A Comment: