Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro , akizungumza na Waislam wa Kata ya Mtinko wakati wa harambee ya ujenzi wa msikiti iliyofanyika Septemba 3, 2023.
................................................
Na Dotto Mwaibale, Singida
WADAU mbalimbali wameombwa kuchangia ujenzi wa Msikiti wa Jaamigh uliopo
Kata ya Mtinko Wilaya ya Singida, mkoani Singida ambapo jumla ya Sh. Bilioni
1.8 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa msikiti huo.
Katibu wa kamati ya ujenzi wa msikiti huo, Abdallah Rajab akizungumza
wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa msikiti huo mbele ya Sheikh wa Mkoa wa
Singida, Issa Nassoro alisema hadi kukamilika kwa ujenzi huo Sh.Bilioni 1.8
zinahitajika.
Rajab alisema msikiti wa awali ambao ulijulikana kama Msikiti wa Ijumaa Mtinko
ulijengwa mwaka 1949 ukiwa na uwezo wa kuhudumia waumini 100 kwa wakati mmoja.
Alisema kutokana na ongezeko la waumini msikiti huo ulipanuliwa mwaka 1990
na kuwa na uwezo wa kuwahudumia waumini 300 na unatumika hadi hivi leo.
Rajab alisema kutokana na ongezeko la waumini na kuanza kuswalia nje mwaka
2018 ndipo walipopata wazo la kuanzisha ujenzi wa msikiti wa sasa wa ghorofa
ambao ujenzi wake ulianza mwaka 2019.
'' Ujenzi upo hatua ya kusuka bimu kwenye msingi na ukikamilika utakuwa na
uwezo wa kuhudumia waumini 1000 kwa wakati mmoja,'' alisema Rajab.
Alisema msikiti huo utakuwa na huduma za ofisi ya utawala, madrasa, vibanda
vya biashara na huduma ya vyoo.
Alisema mahitaji makubwa ya hivi sasa ya ujenzi huo ni mchanga, saruji na
nondo na kuwa katika hatua hiyo waliyoifikia ya ujenzi zimetumika Sh.Milioni
28,059,300 fedha zilizotokana na sadaka za waumini na wadau wengine mbalimbali
na kuwa kwenye akaunti yao wana Sh.Milioni 3.
Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo iliyoandaliwa na uongozi wa msikiti
wakishirikiana na kamati ya bodi ya msikiti, Jumuiya ya Wanawake wa Wakiislam }
JUWAKITA }, wa kata hiyo na kamati ya ujenzi ilifanyika harambee ambapo
zilipatikana zaidi ya Sh.Milioni 3.7.
Katika kuongeza nguvu ya kupatikana kwa fedha za ujenzi wa msikiti huo Sheikh
wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro anatarajia kufanya harambee nyingine hivi
karibuni katika tarehe itakayo pangwa ambayo itawashirikisha wadau na viongozi
mbalimbali wa ndani na nje ya Mkoa wa Singida.
Kamati ya ujenzi wa msikiti huo inawaomba wadau mbalimbali kusaidia ujenzi huo na kwa mtu yeyote, wafanyabiashara, taasisi watakaokuwa tayari kuchangia chochote walichonacho iwe saruji, kokoto, mchanga na vifaa vingine vya ujenzi na kama ni fedha wanaweza kuweka katika akaunti namba 0152737109500 Benki ya CRDB Mtinko Masjid au wanaweza kuwasiliana na Mtunza fedha wa msikiti huo Said Salim Mdimi kwa namba ya simu 0788778591 kwani kutoa ni moyo na si utajiri.
Post A Comment: