Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akiwakabidhi chakula Wafugaji wa Jamii ya Kimasai kutoka Ngorongoro mkoani Arusha walipofika jimboni humo Septemba 17, 2023 kuomba msaada wa chakula.

......................................................................


Na Dotto Mwaibale, Singida

WAFUGAJI Tisa akiwamo mtoto mdogo wa jamii ya Kimasai wametua katika Jimbo la Singida Mashariki lililopo wilayani Ikungi mkoani Singida linaloongozwa na Miraji Mtaturu baada ya kupata taarifa kuwa mwaka jana mbunge huyo alikuwa akitoa msaada wa chakula.

Wamasai hao waliwasili mjini Ikungi wakitokea Kata ya Inokanoka Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na kupokelewa katika kitongoji cha Misri Kijiji cha Ikungi ambapo waliuliza watawezaje kumuona Mbunge Mtaturu.

Wafugaji hao ambao walikuwa katika hali ya kudhoofu kutokana na njaa na safari ndefu, mwenyeji wao aliyewapokea aliyetambulika kwa jina la Hanifa Mwiko ‘ maarufu Mama Saiduni’  aliwapatia chakula kabla ya kwenda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa kitongoji hicho ambaye naye alikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi.

Baada ya polisi kujiridhisha kuwa wageni hao walikuwa na nia ya kumuona Mbunge Mtaturu mwenyeji wao Mama Saiduni aliwapa chumba ambapo walilala hadi siku iliyofuata ambayo mbunge huyo alifika akitokea bungeni Dodoma na kuzungumza nao na baadae kuwapa msaada wa chakula.

Mama wa familia hiyo ya jamii ya kimasai alisema wao walikuwa hawamjui  Mbunge Mtaturu walikuwa wakilijua jina lake tu baada ya kusikia alipokuwa akiwasaidia watu chakula mwaka jana.

"Tulikuwa hatumfahamu Mtaturu tulikuwa tunalijua jina lake tu baada ya kusikia ni mtu mwema na  anawasaidia watu kuwapa chakula kutokana na kuishi bila ya kula kwa kukosa chakula tukaona tuje tumtafute kwani tuliambiwa ni mbunge wa Igunga lakini watu walitueleza kuwa ni wa Ikungi," alisema  mama huyo wa Kimasai.

Mama huyo alisema kufuatia nyumbani kwao kuwa na hali ngumu ya maisha wanaomba hata wapewe vibarua vya kulima na kazi nyingine ili waweze kupata fedha za kujikimu kimaisha.

Akizungumza na wananchi hao Septemba 17, 2023 baada ya kuwapatia chakula Mtaturu aliwapa pole kwa safari ndefu hadi kufika Ikungi lakini aliwaomba mara baada ya kufika nyumbani kwao waende eneo la Msomera wilayani Handeni mkoani Tanga ambalo wametengewa na Serikali na kuwekewa miundombinu mizuri kwa ajili ya kuishi na kupata mahitaji muhimu ya kibinadamu.

"Ninyi wenyewe mmekiri kuwa eneo mnaloishi hamuwezi kufanya kilimo na hakuna huduma niwaombe mkirudi nendeni mlikotengewa na Serikali itakuwa rahisi kusaidiwa," alisema Mtaturu.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Ikungi walimpongeza Mbunge Miraji Mtaturu kwa hatua ya haraka aliyoichukua ya kutoka bungeni Dodoma kwenda Ikungi kuonana na wageni hao na kuwafanyia kitendo hicho cha huruma kwa kuwapa msaada huo kwa kuangalia zaidi utaifa kwani ingekuwa kwa watu wengine wangeweza kuwaacha tu waende zao bila ya kuwasaidia.

Aidha, alipongezwa Mama Saiduni kwa moyo wa upendo wa kuwapokea wageni hao na kuwapa mahali pa kulala na jinsi alivyowasiliana na viongozi wa kitongoji hicho na baadae kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi kwa ajili ya tahadhari na usalama.

Mbunge wa Jimbo la Singida, Mashariki, Miraji Mtaturu kipenzi cha Wananchi wa jimbo lake na maeneo mengine ya nchi akiwa katika moja ya mikutano yake wilayani Ikungi.

 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: