Na. Damian Kunambi, Njombe.
Mradi wa uandaaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji 16 wilayani Ludewa mkoani Njombe umeendelea kutambulishwa kwa wananchi wa vijiji hivyo huku miongoni mwa vijiji hivyo vikiwa tayari vimekwisha pitisha mpango wa matumizi bora ya ardhi.
Mradi huo utakaodumu kwa kipindi cha miaka 10 na kuwawezesha wananchi hao kupata maendeleo sambamba na kuepuka migogoro mbalimbali ya ardhi pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji umepokelewa vyema na wananchi ambapo wameweza kuunda kamati za Halmashauri ya kijiji na kupatiwa mafunzo na maafisa mbalimbali wa Tume ya matumizi bora ya ardhi kutoka jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kutembelea mikutano ya utambulisho wa mradi pamoja na mafunzo ya kamati za halmashauri za kijiji, Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amepongeza utendaji kazi wa maafisa hao na kuongeza kuwa lengo lake ni kuona vijiji vyote vya jimbo lake linakuwa katika mpango mzuri pamoja kutokuwepo kwa migogoro ya mipaka na ardhi.
Kamonga aliiomba Tume hiyo kukamilisha utekelezaji wa zoezi hilo mpaka kufikia upatikanaji wa maendeleo yaliyopangwa na si kuishia katika hatua ya upimaji tu pasipo utekelezaji.
"Naishukuru serikali kwa kuleta mradi huu jimboni kwangu kama nilivyo uomba kwani utakwenda kuleta mabadiliko kwa wananchi kwakuwa kila mmoja wao anayemiliki ardhi ama shamba atakwenda kupatiwa Hati ya umiliki wa ardhi hiyo," Amesema Kamonga.
Nao maafisa hao akiwemo Rehema Mwakinyaka wamesama mpango huo umelenga katika ugawaji wa matumizi hayo ya ardhi unaenda kugawa ardhi kwaajili ya matmizi ya soko, uwekezaji, , stendi ya magari,kilimo,ufugaji na mengineyo hivyo amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi.
"Wilaya zilizo bahatika kunufaika na huu mradi ni wilaya chache hapa nchni ikiwemo wilaya ya Ludewa, hivyo ni vyema wananchi wanapoitwa kutambulishiwa mradi ama kujulishwa mapendekezo ya kamati ya halmashauri ya kijiji ilichopendekeza ni vyema wakajitokeza kwa wingi na kwa muda muafaka ili tuweze kujadili maendeleo haya kwa pamoja". Amesema Mwakinyaka.
Aidha kwa upande wao wananchi wameipongeza serikali pamoja na mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph kamonga kwa kuwafikishia mradi huo na kwamba watahakikisha wanatimiza lengo la mradi na kupata maendeleo.
Post A Comment: