Na Immaculate Makilika - MAELEZO
Wakazi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba Wilaya Mtwara Vijijini wamefurahishwa na uamuzi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakuitaka Bandari ya Mtwara kuanza kusafirisha korosho.
Akizungumza leo wilayani humo katika mahojiano maalum na Afisa wa Idara ya Habari -MAELEZO, Mkazi wa Nanyamba na Mkulima wa korosho, Bw. Burhan Mwema anaeleza kuwa uamuzi huo wa Rais Samia utawanufaisha zaidi wakulima kwa kuwa awali iliwapa ugumu kusafirisha korosho kwa kutumia Bandari ya Dar es salaam.
" Napongeza sana Mhe. Rais kwa hili, itatusaidia sisi hata kujua kinachoendelea kuhusu korosho zetu, kwa kuwa tutaona kila kitu kuliko ilivyokuwa inaenda huko mbali".
Mkulima wa korosho, Ahmed Mchila anasema "Kwanza nimefurahishwa na uamuzi huu wa kutumia Bandari ya Mtwara kusafirisha korosho, hii bandari ipo karibu nasi hapa tutaweza kufuatilia kwa karibu zaidi kila kinachoendelea. Pia, kusafirisha kwa bandari yetu itasaidia hata uzito kutopungua tofauti na tukipeleka mbali muda unavyotumika zaidi katika kusafirisha na korosho zetu zinapungua uzito na bei pia inapungua". Amebainisha Mchila.
Naye, Mbaraka Said anasema " Kusafirisha korosho kupitia bandari yetu hapa itasaidia kuchochea uchumi wa Mtwara kwa kuwa hata wanunuzi kutoka mbali watafika na wakiwa hapa watafanya shughuli mbalimbali zitakazochochea uchumi wetu"
Aidha, Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan jana akizungumza na wananchi wa Mtwara katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona ameeleza "Nimeona eneo jipya la bandari ambalo limejengwa na Serikali. Bandari ile haijajengwa kupamba Mji wa Mtwara. Bandari ile imejengwa kutoa huduma za usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa, kutoka Mtwara na kuingia Mtwara".
"Kilio chenu wananchi ni suala la korosho, kwamba korosho sasa isafirishwe kutokea Bandari ya Mtwara. Mimi sielewi ni nini kinawazuia Mtwara kutosafirisha pale Korosho". Amebainisha Mhe Rais Samia.
Amesisitiza "Niwaombe sana Wanamtwara hasa viongozi, yale ambayo yalikuwa yanazuia Korosho kusafirishwa kupitia bandarini kaeni mkubaliane. Najua kuna wafanyabiashara wenye malori ambayo ndio wanapakia korosho kupeleka Mjini au Dar es Salaam. Lakini kuna wenye vituo vya mafuta, korosho ikisafirishwa kwa meli hawatapata fursa ya magari kujaza mafuta".
Mhe. Rais Samia ameendelea na ziara yake mkoani Mtwara, ambapo mapema leo amezungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara eneo la Nangururuwe na Nanyamba na kisha kuelekea Uwanja wa Majaliwa Tandahimba kwa ajili ya kuzungumza na wanachi wa eneo hilo.
Post A Comment: