WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuthamini, kutambua na kuheshimu mchango wa madhehebu ya dini katika kuimarisha utoaji na upatikanaji wa huduma bora za jamii kwa wananchi.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Septemba 3, 2023) alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Mteule Thomas John Kiangio, Askofu wa Jimbo la Tanga iliyofanyika kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Antony wa Padua lililopo Chumbageni jijini Tanga.
Waziri Mkuu ametoa rai kwa viongozi wa dini, waamini na Watanzania kwa ujumla wazidishe upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa jamii ya Watanzania kwa sababu asili ya dini ni upendo kwa Mwenyezi Mungu na kwa mwanandamu. “Hivyo basi, uwepo wa upendo ni msingi mzuri wa kuendelea kulinda amani tuliyonayo katika Taifa letu.”
Waziri Mkuu amesema hayo yote yasingeweza kufanyika kama Taifa letu lingekuwa katika hali ya machafuko. “Hata leo tumeshiriki kwenye misa hii kwa utulivu kabisa kutokana na amani iliyopo. Sina shaka kuwa mtakubaliana nami kuwa Watanzania wote ni wacha Mungu, wanaotii sheria za Mungu na zile za Serikali na wanatambua wajibu wao wa kiroho wa kutii mamlaka zilizopo.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt. Samia ni kinara katika suala la maridhiano. “Tunayo bahati ya kuwa na Serikali inayosikiliza, inayosimamia haki,uhuru,misingi ya demokrasia na utawala bora wa sheria.”
“Tumeona dhamira njema ya Mheshimiwa Rais, kwa kutenga muda wa kukutana na makundi mbalimbali ikiwemo Baraza la Maaskofu. Nitoe wito kwetu sote kutumia uhuru tuliopewa lakini tukizingatia mipaka ili kendelea kudumisha amani na demokrasia hapa nchini.”
Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru sana viongozi wa madhehebu ya dini kwa kuiunga mkono Serikali katika kutoa huduma kwa jamii ya Watanzania kwani wamekuwa wakiwasaidia watu wenye uhitaji, wamekuwa walezi kwa vijana na yatima pamoja na kutoa huduma kwa wagonjwa tena bila kujali tofauti za kiimani.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa uhusiano kati ya Serikali na madhehebu ya dini umekuwa kutokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya kuendelea kushirikiana na dini zote katika kukuza ustawi wa wananchi kijamii na kiuchumi. “Ushirikiano uliopo katika ya madhehebu ya dini na Serikali umechagiza katika kuimarisha maisha ya Mtanzania mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.”
Askofu Thomas John Kiangio alizaliwa tarehe 17 Machi, 1965 katika kijiji cha Mazinde Ngua wilayani Korogwe, Tanga anakuwa askofu wa tano baada ya kifo cha aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Tanga, Hayati Askofu Anthony Banzi aliyefariki tarehe 20 Desemba, 2020.
Askofu Kiangio amewahi kushika nafasi za kichungaji katika Parokia ya Ekaristi Takatifu huko Lushoto na pia amehudumu katika nafasi ya Msimamizi wa Jimbo Katoliki la Tanga kuanzia mwaka 2020 hadi 07 Juni 2023 alipoteuliwa kuwa Askofu Mteule. Pia amewahi kutumikia katika nafasi ya Gombera Msaidizi (Rector).
Post A Comment: