Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Mhandisi. Peter Ulanga (kulia,) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Uganda (NITA-U) Dkt. Hatwib Mugasa wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa kuunganisha mkongo wa Taifa wa mawasilisho na miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Uganda hafla iliyofanyika leo katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (kulia,)  akimkabidhi zawadi Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa kitaifa wa Uganda Dkt. Chris Baryomunsi (kushoto,) mara baada ya hafla hiyo iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa kuunganisha mkongo wa Taifa wa mawasilisho na miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Uganda na kueleza kuwa utekelezaji wa wa mradi huo utachochea shughuli za kiuchumi na kijamii kidigitali kwa wananchi..Leo jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye akiwakabidhi zawadi baadhi ya wabunge wa Bunge la Uganda waliohudhuria hafla hiyo leo jijini Dar es Salaam.

 KATIKA kuongeza jitihada za kukuza uchumi pamoja na matumizi ya teknolojia kwa wananchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla zaidi ya shilingi Bilioni 71 zimetumika katika uwekezaji wa kuunganisha mkongo wa Taifa wa mawasilisho wa Tanzania na miundombinu ya ya mkongo wa Taifa wa Uganda.


Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa kuunganisha mkongo wa Taifa wa mawasilisho na miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Uganda Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema ushirikiano huo ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Uganda ambapo alikutana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni na kuzungumza namna ya kuboresha sekta ya mawasilisho na TEHAMA kwa ujumla kwa manufaa ya wananchi wa ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Waziri Nape amelitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) ambao ni wasimamizi wakuu wa mradi huo kutoa huduma kwa kuzingatia matakwa ya mkataba huo uliosainiwa na Shirika hilo pamoja na Mamlaka ya Teknolojia ya Habari ya Kitaifa ya Uganda na kusisitiza kutotokea kwa malalamiko ya kukatika katika kwa mtandao.

Aidha ameishukuru Uganda kwa kuichagua Tanzania kupitia TTCL kwa  kutumia mkongo wa Taifa wa mawasilisho na kuitaka TTCL kuziangalia changamoto zitakazojitokeza kwa haraka kwa kuwa mradi huo ni kwa manufaa ya wananchi katika sekta ya TEHAMA hususani vijana na wanawake ambao wanajishughulisha na shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake Waziri wa TEHAMA na Mwongozo wa kitaifa wa Uganda Dkt. Chris Baryomunsi ameeleza kuwa uhusiano baina ya Nchi hizo mbili unazidi kukuwa zaidi na utaendelea kudumishwa kwa manufaa ya vizazi vya mataifa hayo mawili.

Amesema, makubaliano hayo yatumiwe kama fursa ya kiuchumi katika sekta ya mawasilisho na biashara hususani katika kundi kubwa la vijana barani Afrika.

Pia amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) kwa kuendeleza mahusiano hayo.

Vilevile Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Uganda (NITA-U,) Dkt. Hatwib Mugasa amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutashusha gharama za mawasiliano kwa asilimia 50 na kutachagiza ukuaji wa uchumi kupitia fursa mbalimbali kupitia TEHAMA.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL,) Mhandisi Peter Ulanga alieleza kuwa mkataba huo ni wa miaka 15, na  kuunganishwa kwa mkongo wa Taifa wa mawasilisho na miundombinu ya mkongo wa Taifa wa Uganda utafanyika katika mpaka wa Mtukula.

Mhandisi Ulanga ameeleza kuwa Shirika hilo lipo tayari katika utekelezaji wa mradi huo ambao utaibua fursa za kijamii na kiuchumi.

Share To:

Post A Comment: