MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imetoa mafunzo kwa wakulima ili waweze kutumia viuatilifu vilivyosajiliwa kwa usahihi.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mratibu wa Mafunzo kutoka TPHPA, Jumanne Rajabu Jumanne, huku akibainisha kuwa wafanyabiashara, watafaidika kuweza kusambaza viuatilifu sahihi na kutoa taarifa na maelekezo sahihi ya namna ya kutumia viuatilifu
Amesema katika mafunzo hayo ya huduma wima kuhusu matumizi sahihi na salama ya viautilifu yataweza kusaidia wakulima na wafanyabiashara na sekta ya kilimo itakuwa.
Rajabu amesema mafunzo yanayotolewa na mamlaka hiyo kwa wakulima, yatawawezesha kutumia viuatilifu kwa usahihi na kutambua viuatilifu vilivyosajiliwa Tanzania na Mamlaka ya TPHPA kwa sababu viuatilifu vilivyosajiliwa ndivyo vilivyohakikiwa kisayansi kukidhi matakwa ya usalama wa afya ya binadamu, wanyama au mazingira na ufanisi katika kudhibiti visumbufu.
"Katika kutumia viuatilifu, kupitia mafunzo wakulima wanaweza kujua kanuni bora za unyunyiziaji na upuliziaji wa viuatilifu ikiwa ni pamoja na uchaguzi sahihi wa vifaa vya kunyinyizia," amesema.
Amesema idadi kubwa ya wakulima wanawategemea wafanyabiashara kupata maelekezo ya kutumia viuatilifu, hivyo mafunzo hayo yataongeza wigo mpana.
Rajabu amesema maafisa kilimo; wataongeza ujuzi wa kutambua shabaha kwenye maeneo mahususi ya mimea, ili kutoa maelekezo sahihi ya kudhibiti visumbufu kwa kutumia viuatilifu na mbadala sahihi kwa ajili ya ufanisi katika kudhibiti visumbufu ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo
"Watumiaji wote wa viuatilifu wataweza kujikinga kwa kutumia vifaa sahihi vya kuzuia viuatilifu kuingia mwilini kwa kuwa viuatilifu ni kemikeli zenye madhara kiafya," amesema.
Post A Comment: