Na. Anangisye Mwateba-Muheza Tanga


Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula ameutaka uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuwa na mikakati ya kusambaza miche ya miti ya matunda katika maeneo ya shule za Sekondari na Msingi nchini.

Mhe. Kitandula ameyasema hayo akiwa kwenye ziara ya Kutembelea shamba la Miti Longuza na Hifadhi ya Msitu wa Asili Amani wilayani Muheza Mkoani Tanga.

Mhe. Naibu Waziri pia ameutaka uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuanzisha vilabu vya malihai kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ili Watoto na vijana wajifunze umuhimu wa uhifadhi wa malisili za misitu nchini.

Pia Mhe. Kitandula ameutaka uongozi wa Shamba la Miti Longuza kuweka mkakati wa kusambaza zao jipya la miti inayozalisha zao la mpira kwa vijiji ambavyo vinazunguka eneo la shamba hilo kwa kuwapa elimu wananchi wajiunge kwenye kilimo cha miti hiyo.

Vilevile Mhe. Kitandula ameitaka TFS kuboresha hostel na Kuongeza vitanda kwa ajili ya watalii ambao watahitaji kulala kwenye Hifadhi ya Msitu wa Asili Amani ili kuunga juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma katika sekta ya Utalii.

Mhe. Kitandula pia amewataka viongozi wa shamba la Miti Longuza na Hifadhi ya Msitu wa Asili Amani kuwaandaa wananchi na mkutano wa wadau wa mazao ya Nyuki utakao fanyika mwaka 2027 jijini Arusha.

“Fursa za mazao yatokanayo na nyuki  sio asali na Nta peke yake wafundisheni wananchi mazao mengine yanayotokana na ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kunyanyua kipato chao”

Akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mhe. Juma Irando moja ya changamoto inayowasumbua,  ni wananchi kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji ambavyo viko  katika  Hifadhi ya Msitu wa Asili Amani kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja uchimbaji wa madini.

Hivyo rai yake ni kuwa Wakala wa Huduma za Misitu kuendelea kutoa elimu zaidi ya uhifadhi katika Msitu wa Amani ndio chanzo kikuu cha maji yanayotumika katika Mji wa Muheza.



Share To:

Post A Comment: