Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imelipongeza Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwa utendaji kazi mzuri na kuliagiza kupanua wigo wa utoaji wa huduma za viwango na ubora kwa kuanzisha Maabara kikanda nchini ili kuwarahisishia wafanyabiashara kupata huduma hizo kwa urahisi na kuwawezesha kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mariam Ditopile (Mb.) Septemba 09, 2023 wakati Kamati hiyo ilipotembelea Shirika la Viwango Tanzania (TBS) jijini Dar es Salaam ili kupata elimu kuhusu majukumu mbalimbali inayoyatekeleza.
Aidha, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ameipongeza Serikali na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kusimamia uwekezaji wa Maabara za kisasa na viwango vinavyohitajika kimataifa ili kuwawezesha walaji kupata huduma na bidhaa bora zenye usalama pamoja na udhibiti wa bidhaa hafifu zinazoingizwa nchini.
Aidha, Wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha utoaji wa huduma za viwango na ubora kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kushindana katika soko la ndani na nje ya nchi na kuhakikisha Walaji wanapata bidhaa na huduma bora na salama kwa afya zao na maisha yao kwa ujumla.
Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe(Mb.) ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara yake itayafanyia kazi maoni na mapendekezo hayo ikiwemo kupitia na kurekebisha Sera, Sheria na Mikakati inayohusiana na Sekta ya Viwanda na Biashara ili kuhakikisha huduma zinazotolewa na TBS zinaendana na wakati na mabadiliko ya teknolojia.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS Dkt.Athuman Yusuf Ngenya amesema Shirika hilo lina jukumu la kuandaa viwango na kusimamia ubora wa bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na zile zinazotoka nje ya nchi ili kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa sokoni zinakidhi matakwa ya viwango ili kulinda afya, usalama na nakuziwezesha kushindana katika soko la ndani na la kimataifa, hivyo kuchochea maendeleo ya uchumi.
Post A Comment: