Ujumbe wa Tanzania Nchini Thailand ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo, umejifunza namna ya kuendesha Minada ya Kimataifa ya Madini ya Vito kutoka Kampuni kubwa ya Bonas Group ya Ubelgiji yenye uzoefu wa miaka 150 katika shughuli hizo.
Akizungumzia lengo la kushiriki katika mnada huo, Mbibo amesema ni kuona namna kampuni hiyo inavyoendesha minada ya kimataifa ambapo wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali duniani hufika kwa ajili ya kuangalia na kununua madini ghafi, yaliyokatwa na kung'arishwa kutoka nchi mbalimbali duniani zinazozalisha madini ya vito Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi hizo.
Ameongeza kwamba , Wizara imeendelea kupata uzoefu wa namna ya kuendesha minada hiyo kwa tija ikiwemo kutafuta wadau wa kuiendesha ikiwa ni maandalizi ya kuirejesha tena baada ya kuisitisha kwa muda pamoja na kurejesha upya maonesho ya Madini ya Vito na Usonara maarufu kwa jina la Arusha Gem and Jewerly Fair yaliyokuwa yakifanyika kila mwaka.
Mbali na kujifunza kuhusu uendeshaji wa minada ya madini ya vito, tayari ujumbe huo umepata wasaa kujifunza nchini humo kuhusu mnyororo mzima wa shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na bidhaa zake kutoka viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ikiwemo kuangalia teknolojia zinazotumika kuchoma madini ya vito ili kuongeza ubora, kutafuta fursa za kibiashara na uwekezaji na kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
Aidha, ziara hiyo kwa namna moja ni utekelezaji wa baadhi ya vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 ambavyo ni pamoja na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini, uanzishwaji wa minada na maonesho ya madini ya vito.
Kufuatia uzoefu huo, Mbibo ametoa wito kwa watanzania hususan wafanyabiashara na wachimbaji wa madini wenye mawe ya thamani ya vito kujiandaa kikamilifu kushiriki katika minada hiyo ambayo itatoa nafasi ya kuwakutanisha na wanunuzi wakubwa kutoka maeneo mbalimbali duniani.
‘’Tumekutana na mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Bonus Group na baadhi ya watumishi wa kampuni hiyo tumewauliza ni mnada upi unafanya vizuri kati wa huu wa Thailand na Dubai wametueleza ni huu kwasababu una watu wengi wanaotoka mataifa mengi zaidi. Bila kufika kwa watu kama hawa kujifunza, kuona na kuwakaribisha kushiriki, minada itabaki kuwa ya kwetu. Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu imekwisha ruhusu tuanzishe minada na ndiyo sababu tuko hapa kujifunza zaidi,’’ amesema Mbibo.
Kwa upande wake, Meneja wa Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini George Kaseza amesema ziara hiyo ikijumuisha wataalam imelenga kujifunza namna kampuni hiyo inavyopata wanunuzi, inavyotangaza masoko na fursa mbalimbali kupitia madini ya vito na hivyo kutoa mwelekezo mzuri kwa Tanzania kujua namna ya kuendesha minada ya kimataifa ya madini ya vito.
‘’Tuko hapa Bangkok kama wataalam kujifunza namna minada ya madini ya thamani kubwa yanavyofanyika , tunajifunza namna fursa hizi zinavyotumika duniani kote. Sisi wajibu wetu ni kuangalia wenzetu wanavyoendesha minada hii na kutangaza vito. Tuko kujifunza ili tuifanye kuwa bora kwa manufaa ya nchi yetu,’’ amesema Kaseza.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bonus Group Bw. Philip Hoymans amesema kampuni hiyo ipo kuzisaidia nchi wazalishaji na kampuni za madini ya vito kutangaza masoko ili kuongeza thamani ya madini yao na kuongeza ushindani katika ununuzi wa madini ya vito, kupitia zabuni za minada ya madini.
Ameongeza kwamba, minada hiyo inalenga kuweka mazingira ya biashara ya madini ya vito katika sura ya kimataifa ikiwemo kutafuta wanunuzi kupitia taratibu za zabuni.
‘’Leo tunaendelea na zoezi la zabuni ya madini ya vito aina ya Emeralds ya Kampuni ya Belmont Emeralds kutoka nchi ya Brazil, kampuni yetu imekuwa kwenye shughuli hizi kwa miaka 150 sasa na ni furaha kwetu kuukaribisha ujumbe wa Tanzania kuona na kujifunza kwetu, ‘’ amesema Philip.
Katika hatua nyingine, ujumbe huo umekutana na Rais wa Shirikisho la Vyama Vya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito na Bidhaa za Usonara nchini Thailand (TGJTA) Bw. Somchai Phornchindarak na viongozi waandamizi wa umoja huo akiwemo Makamu Rais wa Shirikisho hilo Bw. Chomphol Phornchindarak.
Akizugumza baada ya kikao hicho, Mthaminishaji Mkuu wa Serikali wa Madini ya Almasi na Vito (GDV) kutoka Wizara ya Madini Archard Kalugendo amesema pande hizo zimekubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwemo mafunzo, teknolojia na biashara.
‘’Ametuambia, kuhusu umuhimu wa kushirikiana nao kama wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wa Tanzania katika biashara ya madini ya vito na bidhaa za usonara. Tumewaalika wafanyabishara kutoka Thailand ambao ni wanachama wake ili washirikiane na wenzetu. Mambo makubwa tumekubaliana kushirikiana katika kufundisha vijana, teknolojia na biashara.
Kama unavyojua wenzetu wana biashara kubwa sana ndiyo wanaongoza kwenye biashara ya usonara na kuuza madini ya vito duniani. Tumewaalika pia kushiriki katika Minada ya Madini ya Vito na Maonesho ya Madini ya Vito ya Arusha (AGF), pindi itakapoanza na kushiriki Jukwaa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini mwezi Oktoba,’’ amesema Kalugendo.
Vilevile, ujumbe huo umekutana na Uongozi wa juu wa Chuo cha Mafunzo ya Vito na Usonara cha Serikali cha nchini humo (GIT) ambapo pamoja na mambo mengine, viongozi wa pande zote wamezungumzia namna ya kushirikiana na Serikali kupitia Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha nchini ili kuwapatia mafunzo vijana wa kitanzania kujifunza masuala ya uongezaji thamani madini ya vito kwa ubora kwa lengo la kuchochea shughuli za uongezaji thamani madini nchini, kurithisha ujuzi wa shughuli hizo kwa kizazi kijacho pamoja na kuzalisha ajira ili hatimaye madini hayo yalete manufaa zaidi kwa taifa.
Post A Comment: