Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Idara ya Mahusiano kwa Jamii (Ujirani Mwema) katika Hifadhi ya Taifa Ruaha imekabidhi vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 31 kwa ajili ya mradi wa maji safi na salama unaotarajia kuanza hivi karibuni ili kumtua mama ndoo kichwani na kumpunguzia hadha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo. Zoezi la kukabidhi vifaa hivyo limefanyika leo tarehe 31.08.2023 katika kijiji cha Tungamalenga kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Vifaa hivyo vilivyonunuliwa na TANAPA ni pamoja na mipira ya kupitishia maji (GS Pipe medium na Polly pipe 63 mm) kwa ajili ya kutandazia chini zaidi ya kilometa 2 na vifaa vingine vya mradi wote. Wanufaika wa mradi huo wamechangia nguvu kazi kwa kuchimba mitaro na shilingi milioni 3.2. Shirika linaamini mradi huo utakapokamilika unapunguza changamoto ya ukosefu wa maji katika kijiji hicho.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema "ninayo furaha kubwa kutoa vifaa hivyo ikiwa ni faida inayotokana na utalii, hivyo naahidi kushirikiana nanyi hadi mradi huu utakapokamilika."

"Kwa takribani miaka 12 TANAPA imetekeleza miradi mingi sana. Kama shirika tumetekeleza miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 13 ikihusisha miradi zaidi ya 327 ya afya, elimu,maji na mpango wa matumizi bora ya ardhi kijiji cha Tungamalenga kikiwa ni miongoni mwa vijiji hivyo. Kwa mantiko hiyo tunawajibika kwa wananchi kutekeleza miradi ili kuwapunguzia adha", alisema Kamishna Meing’ataki.

Hata hivyo, Kamishna huyo aliongeza "tunapokabidhi vifaa hivi tujue msingi wake mkubwa ni uhifadhi. Tunaposhirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wananchi hawa katika uhifadhi na kuibua miradi kama hii, tunapata faraja kama shirika kuona wananchi wanatambua thamani ya Maliasili zao".

Aidha,Naibu Kamishna wa Uhifadhi - TANAPA Steria Ndaga, Mkuu wa Kanda ya Kusini aliwaambia wananchi hao licha ya kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya mradi wa maji, kijiji cha Tungamalenga ni wanufaika zaidi wa miradi mingine ya ujenzi wa madarasa na nyumba mbili za walimu walizojengewa hivyo wailinde na kuitunza, pia aliwataka wawe mstari wa mbele kufichua vitendo vya ujangili vinavyoendelea katika hifadhi hiyo.

Akikabidhi vifaa vya mradi wa maji safi na salama kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe.Veronica Kessy, Katibu Tawala Bw. Michael Semindu alisema, "kukamilika kwa mradi huu utaondoa changamoto ya maji hapa. Najua tanki lililopo lina ujazo wa lita 60000 na lilijengwa takribani miaka 20 iliyopita kipindi idadi ya watu ilikuwa ni chini ya 2500, kwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, kijiji hiki kina zaidi ya wananchi 3600. Niwashukuru Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kutambua adha hii"

Kulingana na taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Afya,mtu mmoja anatakiwa atumie maji lita 50 kwa mahitaji yake yote ya msingi kwa siku. Hivyo uwiano uliopo katika kijiji chaTungamalenga hakikidhi matakwa ya umoja wa Mataifa, hivyo TANAPA imeona ni vema kutekeleza mradi huo ili kutatua adha ya maji safi na salama.

Mmoja wa wanufaika Bi. Jennifer Joseph hakusita kuonyesha furaha na hisia zake aliposema " shida ya maji kwetu ni tatizo kubwa na la muda mrefu, unaenda kuteka maji umbali mrefu ukirudi nyumbani muda wa wanafunzi kurudi kula unakuwa umetimia na hujaanda chakula na kusababisha watoto kurudi shule bila mlo wa mchana. Tunawashukuru TANAPA kwa kutuondolea kero hii".

"Kwa hiki tunachokishuhudia leo cha kukabidhiwa vifaa hivi tunaahidi kuilinda Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa nguvu zetu zote, kwa wale waliokuwa wanakula nyamapori na kuiita mchicha tutawasemea bila woga," aliongeza Bi. Jennifer.

Kijiji cha Tungamalenga ambacho wananchi wake ndio wanufaika wa mradi huo kiko takribani kilometa 20 kutoka Lango kuu la Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Share To:

Post A Comment: