📍Kasulu, Kigoma📍

Shirika la Posta Tanzania limetoa madawati 100 kwa Shule ya Msingi Nyansha, Wilaya ya Kasulu mjini ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi hivyo kutimiza ndoto zao, leo tarehe 23 Septemba, 2023.


Madawati hayo yaliyokabidhiwa kwa Mbunge wa Kasulu Mjini ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako yamekuwa ni sehemu ya kuigusa jamii hasa katika sekta ya Elimu Wilayani humo.

Katika makabidhiano hayo Profesa Ndalichako ameeleza kuwa, kwa sasa Serikali ya Awamu ya sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka vipaumbele katika huduma muhimu za jamii ikiwemo Sekta ya Elimu nchini ambapo elimu ndiyo msingi wa kulitoa taifa letu katika umaskini na kuwajengea uwezo wananchi katika kulikuza Taifa kichumi.

Aidha, Waziri Profesa Ndalichako ametumia nafasi hiyo kulipongeza Shirika la Posta Tanzania kwa kutambua umuhimu wa Sekta ya Elimu nchini na kuchangia madawati hayo 100 kwa Shule ya Msingi Nyansha lengo ikiwa kuweka mazingira wezeshi kwa wanafunzi kujifunza.

Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Isaac Mwakisu ameeleza kuwa Wilaya ya Kasulu ina upungufu wa takribani madawa 22,500 hivyo kwa Shirika la Posta kukabidhi madawati hayo kutaendelea kutatua changamoto ya uhaba wa madawati wilayani humo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Ndg. Dollar Kusenge amelishukuru Shirika la Posta Tanzania kwa kuwa sehemu ya kutatua changamoto ya madawati katika Shule ya Msingi Nyansha na madawati hayo yataongeza chachu kwa wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao.

Akizungumza kwa niaba ya Postamasta Mkuu, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano Bw. Amos Millinga ameeleza kuwa Shirika la Posta linatambua juhudi mbalimbali za Serikali zinazolenga kuboresha sekta ya elimu hivyo Shirika limeona liunge mkono kuboresha mazingira ya elimu kwa wananchi na wadau wa elimu.
 

Imetolewa na;
Kurugenzi ya Masoko na Uhusiano
Shirika la Posta Tanzania,
23 Septemba, 2023.
Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: