WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda ameshukuru mashirika ya Umoja wa Mataifa ya UNESCO na UNICEF kwa kushirikiana na serikali kuandaa muongozo wa elimu kwa ajili ya maendeleo endelevu.


Alisema hayo wakati wa Uzinduzi wa Mpango wa Elimu kwa Maendeleo Endelevu (2023-2030) unaolenga kuhuisha masuala ya hifadhi ya mazingira hususan, kupunguza na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, mjini hapa.

Alisema nchi za SADC kupitia mawaziri wa Elimu walikutana na kuipa Kazi UNESCO ya kuratibu miongozo hiyo kwa nchi zote za SADC. Aidha Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kumaliza uaandaji wa Muongozo huo baada ya kukamilika ndio wamekutana kuupitia kwa ajili ya matumizi.

Alisema kazi yake kuu ya muongozo huo ni kuona Elimu inayotolewa inawaandaa vijana kuelewa changamoto za mazingira, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu kwa ujumla wake.

Prof. Mkenda alisema muongozo huo unaakisi yaliyomo katika Rasimu ya sera ya Elimu na Mafunzo ya Amali 2014 Toleo la 2023 linalotarajiwa kutoka siku za karibuni.

Alisema Muongozo huo ni mkakati wa serikali kwa maendeleo endelevu na ni muhimu sana kwa Dunia inavyoenda kwa sasa.

"Elimu yetu ambayo tunaitoa ya mafunzo ya Amali kwa Sasa hivi tutawaandaa vijana wetu katika mambo ya viwanda na katika masuala mbalimbali yanayoendana na ujasiriamali kwa hiyo tunafurahi hatimaye sisi tunao Muongozo na inawezekana ndio nchi ya kwanza kukamilisha Kazi hii ya Muongozo huu" alisema.

Awali Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Michel Toto alisema UNESCO imeridhika na kushurukuru kushirikishwa katika uandaaji wa Muongozo huo na inayofuraha kuwa sehemu ya kukamilisha zoezi hilo muhimu kwa maendeleo ya bara la Afrika hususani nchi za SADC.

“Zaidi ya hayo, shukrani zetu za kina zinatolewa kwa UNICEF kwa msaada wao wa kifedha, ambao ulichukua jukumu muhimu katika kuandaa mkutano huu muhimu.

Mfumo huu unaonyesha matarajio yetu ya pamoja kwa mustakabali wa elimu katika taifa hili kuu.”

Toto alisema Elimu kwa Maendeleo Endelevu (ESD) ni mwitikio wa sekta ya elimu wa UNESCO kwa changamoto za dharura na kubwa za dunia.

“Shughuli za pamoja za wanadamu zimebadilisha mifumo ya ikolojia ya dunia ili kwamba uhai wetu uonekane kuwa hatarini. Kudhibiti ongezeko la joto duniani kabla ya kufikia viwango vya janga kunamaanisha kushughulikia kwa ukamilifu masuala ya mazingira, kijamii na kiuchumi, “ alisema Toto na kuongeza kuwa mpango wa elimu wa UNESCO wa 2030 unalenga kuleta mabadiliko ya kibinafsi na ya kijamii yanayohitajika ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi” alisema.

Alishukuru Serikali ya Tanzania kwa dhamira yake thabiti ya kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan Lengo Namba 4, linalozingatia Elimu na linajumuisha malengo muhimu ya kuendeleza Elimu kwa Maendeleo Endelevu.

Kwa Upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Salim Abdullah alisema kwamba kwa Upande wa Zanzibar Mpango huo utasaidia kuweka mabadiliko sahihi ya uelewa katika jamiii kwa kushirikisha wanafunzi wangali skuli kupitia mafunzo ya amali.













Share To:

Post A Comment: