Serikali imesema inaendelea na jitihada za kudhibiti mimea vamizi katika maeneo ya Hifadhi na Mapori ya Akiba kwa lengo la kurejesha uoto wa asili nchini ambao ni tegemeo kwa wanyamapori.
Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula wakati akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe.Mohamed Jumah Soud aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kupunguza upoteaji wa uoto wa asili nchini unaosababisha kupoteza hadhi kwa Hifadhi na Mapori ya Akiba.
Mhe. Kitandula ametaja sababu kubwa ya kupotea kwa uoto wa asili katika Hifadhi na Mapori ya Akiba kuwa ni ongezeko la mimea vamizi katika maeneo hayo inayosababishwa na uvamizi wa shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na uingizwaji wa mifugo hifadhini na kwenye mapori ya akiba.
Vilevile vile Mhe. Kitandula amesema mimea hiyo husababisha mabadiliko ya aina ya mimea katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa kutoa fursa kwa mimea isiyoliwa na wanyamapori kustawi zaidi, kuongezeka na kupunguza uoto wa asili ambao ni tegemeo la wanyamapori.
Aidha ameongeza kuwa katika jitihada za kudhibiti mimea vamizi, Wizara kupitia taasisi za uhifadhi inatekeleza Mkakati wa kukabiliana na mimea vamizi katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na kuondoa kwa kung’oa mimea husika katika hifadhi.
Amesema pamoja na mikakati hiyo, tafiti 47 zimebaini mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa hivyo serikali itaendelea kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa kudhibiti shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na uingizwaji wa mifugo hifadhini sambamba na kuwekeza zaidi katika utafiti ili kupata suluhisho la kudumu.
Post A Comment: