Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Serikali ya Wilaya ya Kishapu imesema itaendelea kushirikiana na Kampeni ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii Tanzania SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga katika kuibua na kukemea ukatili unaoendelea kufanyika kwenye jamii.

Hayo yamezungunzwa na viongozi mbalimbali wakati wa ziara ya viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, ambapo leo wametembelea  Wilaya ya Kishapu kwa lengo la kuimarisha uhai wa kampeni hiyo.

Viongozi hao akiwemo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu Bwana Sabinus Chaula, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu Esther Zephania Gesogwe pamoja na kaimu katibu tawala wa Wilaya ya Kishapu Bwana Geven Noah wamewapongeza viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga kwa juhudi wanazozifanya huku wakiahidi kuendelea kushirikiana katika kutokomeza ukatili.

Wamesema jamii katika Wilaya hiyo bado inauelewa mdogo juu ya haki zao za msingi ambapo wamesema baadhi ya familia ukatili bado unaendelea ikiwemo mila na desturi kandamizi, mifumo dume pamoja na ndoa za utotoni.

Wameiomba kampeni ya SMAUJATA Wilaya na Mkoa wa Shinyanga kuendelea kushirikiana na serikali katika jitihada mbalimbali za kupambana na ukatili ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya ukatili, kuandaa mabonanza mbalimbali, kufanya mikutano ya hadhara pamoja na kutembelea familia ili kuibua ukatili unaoendelea kufanyika.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, Mwenyekiti idara ya maadili SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Solomon Nalinga Najulwa jila maarufu Cheupe kempeni hiyo itaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali, wadau mbalimbali pamoja na wananchi katika kuibua na kupambana na ukatili unaoendelea kufanyika kwenye jamii.

Kwa upande wake katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Bwana Daniel Kapaya amewashukuru viongozi hao ambapo amesema kampeni hiyo itaendelea kutoa elimu ya ukatili pamoja na kuibua ukatili kwa lengo la kuhakikisha jamii inakuwa salama siku zito.

Aidha Mwenyekiti wa SMAUJATA Wilaya ya Kishapu Mwalimu Shamika Hilaly Juma naye amesema uongozi wa SMAUJATA Wilaya hiyo utaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali wakiwemo Polisi kitengo cha dawati la jinsia wanawake na watoto kwa kuhakikisha wanaifikia jamii husika ili kuepukana na athari zitokanazo na ukatili.

Viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga leo wamefanya ziara yao ya kikazi Wilaya ya Kishapu na kwamba ziara hiyo ni endelevu ambapo wanatarajia kufanya ziara katika Wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga.

 

 

Viongozi wa SMAUJATA Wilaya na Mkoa wa Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja na katibu wa mbunge jimbo la Kishapu Bwana Godfrey Nchimika Mussa ikiwa ni sehemu ya ziara ya viongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga katika Wilaya ya Kishapu leo Ijumaa Septembe Mos Mwaka 2023.

Share To:

Misalaba

Post A Comment: