Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametoa siku tatu (3) kwa wakazi wa Kata ya Haubi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kuhakikisha wanarudisha anuani za Makazi zilizo wekwa na serikali kwa ajili ya utambulisho ajili kwa Wananchi wote waliotoa huku akiwaeleza hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaoenda kinyume na maelekezo hayo.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 15,2023 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa ya kukagua miradi ya maendeleo na miundombinu mbalimbali katika shule mpya ya Sekondari katika Kata ya Bolisa, Shule mpya ya Sekondari Ntomoko iliyopo katika Kata ya Haubi sambamba na kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Haubi, Ujenzi huo unatekelezwa kupitia Fedha za SEQUIP.
"Kawatangazieni na wengine tunatoa siku tatu kwa yeyote aliyetoa anuani za Makazi ahakikishe anarudisha sehemu husika alipotoa kwa asiyerudisha tutamfungulia mashitaka "amesisitiza Senyamule
Aidha, Kiasi cha zaidi ya shilingi Millioni 544 zimewekwa kwenye account ya Shule ya Sekondari Hubali kwa ajili ya Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Bolisa unaohusisha Jengo moja la Utawala, Vyumba nane vya madarasa, matundu nane ya vyoo vya wanafunzi, Jengo moja la Maktaba, Jengo moja la Tehama pamoja na majengo matatu ya maabara .
Pia, Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ilipokea kiasi cha zaidi ya shilingi Millioni 544 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Ntomoko iliyopo katika Kata ya Haubi, mradi ambao unahusisha ujenzi wa Jengo moja la Utawala, Jengo moja la Tehema, Vyumba viwili vya madarasa na Ofisi moja, katika (BLOCK A na B ), Vyumba viwili vya madarasa (BLOCK C na D), Ujenzi wa madarasa matatu ,Jengo la Maktaba, matundu nane ya vyoo, kichomea taka ,chumba cha mahitaji maalum pamoja na tenki la maji ya ardhini.
Mhe.Senyamule amehimiza suala la Usalama wakati akijibu changamoto mbalimbali za wananchi wa Kata ya Haubi amewataka wazazi na walezi kusimamia malezi ya watoto wao ili kulinda mila na tamaduni pamoja na maadili ya taifa.
"Suala la Usalama linaanza na sisi, tuanze wote kwa pamoja kwa kuchukua hatua za kusimamia malezi mazuri ili nchi yetu isiwe na watoto wabakaji, walawiti, wavuta bangi na mmomonyoko wa maadili." Amesisitiza Senyamule
Mkuu wa Mkoa huyo amewaasa vijana na watu wote wanaojishughulisha na kilimo na biashara ya bangi kuacha mara moja kwani ni kinyume na taratibu za nchini ya Tanzania na kuwaagiza kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake kwa kukemea na kutoa taarifa kwenye vyombo vya sheria.
"Natoa shime mnajua bangi ni kinyume cha sheria na taratibu wengine tayari wapo ndani, kama kuna watu bado wanaweka bangi ndani watumieni salamu, hatutaki vijana wetu waharibikiwe kama kuna wanaolima tuwakemee kwahiyo lazima kila mtu awe mlinzi wa mwenzake." Amesisitiza Mhe.Senyamule
Post A Comment: