Waganga Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Songwe, Katavi, Mbeya, Kigoma na Kagera wametakiwa kukamilisha maandalizi ya kampeni ya Kitaifa ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa Polio inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 21 hadi 24 Septemba 2023 katika Mikoa hiyo ili kuwaongezea kinga watoto.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu alipofanya kikao na watumishi wa Sekta ya Afya Mkoani Rukwa baada ya kukagua maandalizi ya utoaji wa huduma ya chanjo ya polio.
“Niwaelekeze waganga wote wa Mikoa itakayotoa chanjo wafanye maandalizi kabla ya tarehe ya zoezi la chanjo, muhakikishe kwenye vituo vyote vya utoaji chanjo kuna kila kitu kinachohusiana na chanjo na watoa chanjo wapiti nyumba hadi nyumba”. Amesema Prof. Nagu.
Aidha, Prof Nagu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanatoa hamasa kwa wananchi kupitia viongozi wa kidini, watu mashuhuri katika Jamii na kwa kupitia vyombo vya habari na kurasa za mitandao ya kijamii.
Pia, Prof. Nagu ameendelea kusisitiza kufikiwa kwa kila mtoto mwenye umri chini ya miaka Nane pasipo kujali changamoto za kijiografia kwani mikakati iliyowekwa kupitia huduma tembezi ni kuhakikisha chanjo hiyo inawafikia watoto wote wanaoishi katika maeneo ya mbali na maeneo yasiyofikika kwa urahisi kwa kuwa na timu zitakazotoa huduma hiyo.
Hata hivyo, Prof. Nagu amesema kutokana na ugonjwa wa Polio huambukiza kupitia kinyesi hivyo amewataka wananchi wote wakumbushwe na kuelekezwa juu ya kudumisha usafi na matumizi sahihi ya vyoo.
Mwisho, Prof. Nagu ameyashukuru mashirika ya kimataifa, likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na UNICEF, kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Serikali ya Tanzania katika kutokomeza magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Polio.
Post A Comment: