Na. WAF - Songwe
Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) na Halmashauri zote za Mkoa (CHMT) wametakiwa kufanya majukumu yao kwa wakati ikiwemo kufanya maoteo sahihi ya dawa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhee. Ummy Mwalimu Septemba 13, 2023 wakati akiongea na wajumbe wa Timu za Usimamizi na Uendeshaji wa huduma za Afya ngazi ya Mkoa (RHMT) na Halmashauri zote za Mkoa (CHMT) na Wajumbe wa Timu ya Uendeshaji wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa (RRHMT) wakati akihitimisha ziara yake ya siku Tatu katika Mkoa wa Songwe.
“Niendelee kusisitiza kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kupitia CHMT kufanya maoteo sahihi ya dawa, Pili kusimamia matumizi ya dawa na Tatu kuhakikisha mnafanya kaguzi za mara kwa mara za bidhaa za Afya”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatimiza wajibu wake anatoa fedha za dawa kwa asilimia 100 kila Mwaka, hivyo ni wajibu wa viongozi kusimamia upatikanaji wa dawa.
Aidha, katika kuhitimisha ziara yake ya siku Tatu katika Mkoa wa Songwe, Waziri Ummy amesema kwa ujumla hali ya huduma zinazotolewa katika vituo vya Afya pamoja na upatikanaji wa dawa unaridhisha.
“Baada ya kutembelea katika Wilaya ya Songwe (Mkwajuni), Halmashauri ya Wilaya ya Momba na kumalizia ziara yangu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe kwakweli nimeridhishwa na huduma zinazotolewa lakini pia upatikanaji wa dawa”. Amesema Waziri Ummy.
Mwisho, Waziri Ummy amesema Serikali inaangalia ubora wa huduma katika nyanja tofauti ikiwemo upatikanaji wa dawa, upatikanaji wa vifaa tiba, vitendanishi, kauli za watumishi wakati wa kutoa huduma kwa wagonjwa pamoja na ujazaji wa taarifa za Afya kwa kutumia mifumo.
Post A Comment: