Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia inaendelea na mradi wa Kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari nchini unaofahamika kama SEQUIP. Madhumuni ya mradi huu ni kuongeza ufikiwaji wa elimu ya sekondari pamoja na kuwapatia wasichana mazingira bora ya kujifunza na kuboresha uhitimu bora wa elimu ya sekondari kwa wasichana na wavulana.
Mkoani Arusha katika Halmashauri ya Longido ambayo ilitengewa Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya masomo ya Sayansi hali imekuwa tofauti kwani mpaka sasa wameshindwa kuanza ujenzi wa shule hiyo pasipo sababu zozote.
John Mongella ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambapo amefanya ziara katika kijiji cha Oltepes Wilayani Longido panapo jengwa shule hiyo ya wasichana kukerwa na hatua iliyopo na kutoa maelekezo ya kuharakisha ujenzi huo sambamba na kuagiza kufikishwa huduma ya umeme pamoja na maji katika eneo hilo ili kuwezesha kurahisisha ujenzi huo uliopo nje ya muda kwani disemba mwaka huu shule inatakikana kuwa imekamilika.
"Lori linabeba kokote,mchanga au mawe tripu tano kwa siku sasa najua hapa mnatengeneza mazingira ya kuongeza malori mengine ili mtoe nafasi kwa malori yenu,mmeshachelewesha ujenzi wa hii shule halafu mnatafuta sababu nyingine sasa sitaki kusikia hili lori limeharibika na Dc utajua unalilaza wapi" Alisema Mongela
"Ujenzi wa shule hii ulipaswa uanze lakini hela zimefika kuna watu wanahangaika na mambo mengine ili watengeneze mianya yao sasa tengenezeni faili la kila mnachonunua serikali imetoa bilioni 3 kujenga shule hii na wenzenu wengine katika mikoa mingine wanajenga halafu nyie mnakuja na sababu lukuki" Aliongezea Rc Mongela
Sambamba na hilo Rc Mongela alibaini uwepo wa lori la Halmashauri ambalo ni zima lakini linatengenezewa mazingira ya kazi nyingi ili malori mengine yaweze kukodishwa ili hali lori hilo linaweza kusomba mchanga,kokoto na vitu vingine kwa awamu.
Mkuu wa Mkoa amefanya ziara katika Kijiji hicho inapojengwa shule hiyo na kubaini kutokuwepo na hata mchanga wala moramu zilizoanza kumwagwa ingali alikuta mafundi wakihangaika kupimapima huku taarifa kutoka kwa Ofisa Manunuzi, Godless David akidai walitangaza zabuni lakini mzabuni Ngulelo Service Limited mmoja alishinda zabuni zaidi ya nne lakini alikuwa anataka hela ya juu zaidi kuliko kiwango kilichotengwa.
"Fedha iliyotengwa ni ndogo mzabuni anataka bei ya juu zaidi hapa tupo katika hatua ya kuagiza vifaa vya awali na pia hapa tunalori moja lakini mahitaji ni mengi sana "
Kwa uoande wake Mkuu wa Wilaya ya Longido,Marko Ng'umbi alisema atasimamia ujenzi wa shule hiyo ili iweze kukamilika huku Injinia wa mradi huo,Grace Nicodemus alisema wameshachora ramani ya eneo hilo na wapo tayari kuanza kwa ujenzi huo
Hata hivyo Ofisa Elimu Mkoa wa Arusha Abel Mtupwa alisema serikali imetoa bilioni 3 kupitia mradi wa Sequip ambapo ni mradi wa Kuboresha Elimu Nchini ambapo kumekuwa na hali ya kusuasua na inatarajia kukamilika Disemba na itakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi kutoka halmashauri ya wilaya saba za Mkoa wa Arusha na itakuwa ni maalum kwaajili ya wasichana wenye ufaulu wa juu zaidi.
Ikumbukwe Serikali ilitenga Jumla ya Shilingi Trilioni 2.78 kwaajili ya ujenzi wa miundo mbinu ya Elimu ya Msingi na Sekondari kwa kipindi cha Miaka mitano(5) yaani 2022 hadi 2027 kupitia miradi mbalimbali ya Elimu ikiwemo miradi mikubwa mitatu ambayo ni Mradi wa Kuboresha Elimu Sekondari (SEQUIP), Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) na Program ya Kutekekeza Elimu kwa Matokeo (EP4R).
Post A Comment: