Na John Walter-Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga amewatahadharisha wananchi juu ya uwepo wa El-Nino, akiwataka wanaofanya shughuli za kijamii kwenye maeneo ya bondeni na waliojenga katika maeneo hayo kujiandaa kuepuka athari.
Amesema kutokana na El-Nino hiyo ambayo itaugusa mkoa wa Manyara, mvua kubwa zinatarajiwa kuonyesha katika msimu wa vuli mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka huu.
Kwa Mujibu wa  taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini Tanzania (TMA), imesema mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023.
Sendiga ametoa tahadhari hiyo leo Septemba 9, 2023 wakati akiongoza zoezi la usafi wa mazingira katika mitaa mbalimbali ya mji wa Babati ikiwemo soko kuu.
TMA imetaja nyanda za juu kaskazini Mashariki inayohusisha mikoa ya Manyara,Arusha na Kilimanjaro kukumbwa na  mvua hizo kubwa.
Amesema Babati bila uchafu inawezekana hivyo watu wawe na tabia ya kufanya usafi wenyewe na sio kusubiri mkurugenzi apitishe gari la matangazo.
Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange ameagiza taka zinazokusanywa maeneo mbalimbali ziondolewe kwa wakati kuhifadhiwa panapostahili au kuteketezwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Babati Upendo Mangali amesema zoezi la Usafi ni endelevu na kwamba wataendelea kusimamia usafi wa Mazingira na kubaki na sifa iliyopata mwaka jana kuwa mji msafi kati ya miji yote 19 nchini.

 
Share To:

Post A Comment: