Unguja. Tarehe 10 Septemba 2023: Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt Hussein Ali Mwinyi ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha huduma za kibenki zinazofuata misingi ya sharia hivyo kuwahamasisha Waislamu wengi kutumia huduma zake jambo linalochochea ujumuishi wa kifedha.

Rais Mwinyi ambaye alikuwa mteja wa kwanza kufungua akaunti ya Al Barakah mwishoni mwa mwaka 2021 huduma hiyo ilipozinduliwa, ametoa pongezi hizo alipokabidhiwa kadi ya akaunti hiyo mwishoni mwa wiki alipotembelewa na ujumbe wa Benki ya CRDB ikulu mjini Zanzibar.
“Tulijua Al Barakah itakuwa na mafanikio lakini hatukutarajia kuwa yangepatikana ndani ya muda mfupi namna hii. Nawapongeza kwa mafanikio mliyoyapata na niwaahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendeleza ushirikiano na benki yenu kuhakikisha huduma hizi zinawafikia Waislamu wengi walipo visiwani humu ili kwa Pamoja tushiriki kulijenga Taifa letu huku tukimwabudu Mwenyezi Mungu bila kukiuka maagizo yake,” amesema Dkt Mwinyi.

Rais Mwinyi pia ameishukuru Benki ya CRDB kwa heshima iliyompa ya kuwa mteja wa kwanza kukabidhiwa kadi ya Akaunti ya Al Barakah na akasema jambo hilo limemhamasisha zaidi hivyo ataangalia namna ya kuongeza amana kwenye akaunti yake ili kufurahia huduma hizo zinazokidhi mahitaji yake ya kifedha na imani ya kiroho.
Akimkabidhi kadi ya Al Barakah, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Benki ya CRDB inayojumuisha Zanzibar na mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Badru Idd amesema Rais Mwinyi sio tu alihamasisha kuanzishwa kwa huduma hizo bali alionyesha mfano kwa kuwa wa kwanza kufungua akaunti hiyo mwaka 2021 ambayo mpaka sasa ina wateja zaidi ya 70,000 nchini kote.

“Mpaka sasa hivi, tumekopesha zaidi ya shilingi bilioni 90 kwa misingi ya sharia na tumepokea amana za wateja zaidi ya shilingi 85 bilioni ndani ya miaka miwili ya kutoa huduma hizi. Huduma za CRDB Al Barakah Banking zinaendelea kutoa mchango mkubwa sana katika serikali yako ya Zanzibar na wananchi wake kwani tumekopesha zaidi ya shilingi 18 bilioni kwenye uchumi wa buluu na wafanyabiashara wamepata Zaidi ya shilingi bilioni 33,” amesema Idd.

Ili kusogeza huduma kwa wananchi visiwani humu, Benki ya CRDB ilifungua tawi mjini Wete lililozinduliwa na Rais Mwinyi mwaka 2021 alikoiomba benki kuanzisha huduma zenye misingi ya sharia na mpaka sasa, kwenye matawi manne ya Benki ya CRDB yaliyomo Zanzibar, wananchi wameweka amana za zaidi ya shilingi bilioni 28.
Kuhusu kadi za Akaunti ya Al Barakah, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Benki Zinazofuata Sharia (Islamic Bankink) wa Benki ya CRDB, Rashid Rashid amesema zipo za aina nne na zote zinaweza kutumika katika majukwaa yote ikiwamo kwa mawakala zaidi ya 200 waliopo Zanzibar kama ilivyo kwa kadi zinazotumiwa na wateja wengine wote wa Benki ya CRDB.

“Pamoja na mafanikio haya makubwa, CRDB Al Barakah Banking tunaendelea kuboresha huduma zetu ili kuwafikia wateja wetu na kuwapa amani wanayoitegemea kwa kuweka pesa zao katika akaunti za Al Barakah zinazofuatisha misingi ya sharia. Kila mteja mwenye akaunti hii, ana amani kwa kujua kwamba pesa zake ziko mahala salama na zina uangalizi maalum unaoendana na imani na maadili yake,” amesema Rashid.
Akizungumzia umuhimu wa huduma za fedha kwa maendeleo ya Taifa, Mwenyekiti wa Bodi ya Huduma za Fedha Zinazofuata Misingi ya Sharia ya Benki ya CRDB, Abdul van Mohammed amesema kuna fursa nyingi ambazo Zanzibar inaweza kunufaika nazo iwapo itafungua milango.

“Zanzibar ndio yenye matumizi makubwa ya Islamic Banking Afrika Mashariki. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kuifanya kuwa ya kwanza kuuza hatifungani ya Kiislam ili kupata fedha zitakazochangia maendeleo ya watu wetu,” amesema Mohammed.




Share To:

Post A Comment: