Na Dotto Mwaibale,
Iramba
WAKATI kukiwa kumebakiza miaka miwili kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa 2025, Mbunge wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Prof. Kitila Mkumbo ambaye ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji ametangaza rasmi kumaliza tofauti zao za kisiasa na Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye ni Waziri wa Fedha, Dk.Mwigulu Nchemba.
Prof. Mkumbo na
Dk.Mwigulu ambao wote ni wazaliwa wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida walivutana
kugombea ubunge katika jimbo la Iramba Magharibi kabla ya suala hilo kuingiliwa
na aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa enzi hizo hayati Dk. John Magufuli, ambaye
aliamuru Prof. Mkumbo akagombee ubunge Ubungo ili kumuachia Dk. Mwigulu Iramba
Magharibi.
Viongozi hao walimaliza tofauti zao mwisho
mwa wiki wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Henan
Highway Engineering Group Ltd ya nchini
China kuanza kazi ya ujenzi wa barabara ya Singida-Sepuka- Ndago, Kizaga.
Akizungumza katika hafla hiyo Prof. Mkumbo alisema yeye na Dk. Mwigulu
walishamaliza tofauti zao za kisiasa zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu wa
2015.
"Nawaletea
tangazo langu kwamba mimi na Mwigulu tulishayamaliza, hatununiani, hatukasilikiani, tunakaa
pamoja na tunakula nyama pamoja, sasa nyie wengine msidhani bado hatuelewani
mtakuwa vichaa, kwahiyo, hilo limeisha," alisema Mkumbo huku akishangiliwa
na wananchi waliohudhuria hafla hiyo.
Alisema baada ya
mvutano wao kisiasa kufikia tamati kilichobaki ni wananchi wa jimbo la Iramba
Magharibi kuendelea kumuunga mkono Dk. Mwigulu kwa ajili ya kuleta maendeleo ya
Wilaya ya Iramba.
"Mnafahamu kutoka mwaka 2013 hadi 2020 mimi na mdogo wangu (Dk. Mwigulu) tulipambana kisiasa lakini tunamshukru Mungu wote tumekuwa wabunge na mawaziri," alisema Prof Mkumbo na kuongeza kuwa;
"Mimi Mbunge wa
Ubungo, jijini Dar es Salaam, kule kwetu kwenye jimbo langu ukija wazaramo
watakuimbia kwamba muacheni Kitila abaki alipo na mimi nawaambia leo muacheni
Mwigulu abaki pale alipo.""
Prof. Mkumbo alitumia
hafla hiyo kumshukru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini watoto wa Iramba
(Dk. Mwigulu na Prof. Mkumbo) kwa kuwateua kuwa mawaziri.
"Mama (Rais
Samia Suluhu Hassan) ametuamini watoto wenu wawili katukabidhi wizara nyeti za
uchumi wa nchi, kanikabidhi mimi nipange
mipango nikimaliza kupanga mipango nimkabidhi Mwigulu Nchemba atoe fedha, mnataka
nini ? ," Alihoji.
Akizungumza baada ya
Profesa Mkumbo kutoa maneneo hayo Mwigulu alimshukuru na kueleza kuwa
walikwisha maliza tofauti zao siku nyingi kilichobakia ilikuwa ni Mkumbo
kuzungumza mbele ya kadamnasi.
"Mimi na huyu
ndugu yangu tofauti zetu tulikwisha zimaliza siku nyingi na tumekuwa tukishirikiana
kwa mambo mengi na hata hii Shahada ya Udaktari (PhD) niliyonayo ni yeye
aliyenishauri niende nikasome," alisema Mwigulu huku wananchi
wakimshangilia kwa furaha.
Alipopata nafasi ya kuzungumza Mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa aliipongeza hatua hiyo walioichukua viongozi hao na akawataka kufanyakazi kwa bidii kwa maslahi mapana ya wana Iramba na Taifa zima kwa ujumla baada ya kupewa nafasi za juu Serikalini na Rais Samia Suluhu Hassan.
Post A Comment: