Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa Geophrey Pinda ameonya baadhi ya viongozi wanaosababisha migogoro ya ardhi ya mipaka isiyo na tija kwa Taifa.


Pinda amesema hayo wakati alipokutana na Watumishi wa Sekta ya Ardhi mkoa wa Tanga ambapo alibaini kuwa Wizara yake inatatua migogoro mingi ambayo kiundani inasababishwa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri na baadhi ya Viongozi wa Serikali za mitaa.


"Wakati mwingine migogoro mingi ni ya watawala wanaogombea madaraka na mapato, wananchi na mifugo yao hawahitaji hiyo mipaka na wala hawana habari bali wanagombanishwa tu na viongozi" amesema Pinda.


Amesema siku akipata nafasi ya kumshauri Mheshimiwa Waziri Mkuu atamuomba kufanya mabadiliko kwa viongozi wanaogombania mipaka, awabadilishe wa huku aende kule na wa kule arudi huku ili kila mmoja aone alichokuwa anakigombea kwa mwenzie kina manufaa au laa. 



"Wizara ya Ardhi ishaweka alama za mipaka ardhini kwa hiyo kazi ya viongozi ni kutafsiri zile alama ilikuwasidia viongozi wa Serikali za Mikoa, Wilaya na Mitaa kujua mipaka yao ya kiutawala na sio kuwagawa wananchi na shughuli zao. Amesema Pinda.


Aidha, ametaka viongozi wasiwachanganye wananchi kwa kuwachochea na kuwajengea hoja wasimame kudai maeneo bila kuwa na uelewa wa mgogoro wanao jiingiza.


Share To:

ELIZA DOM

Post A Comment: