NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deo Ndejembi amewataka wataalamu wa idara ya elimu kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi kulingana na thamani ya fedha inayotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi na kwamba serikali haitomvumilia mtumishi yeyote atakayeleta uzembe kwenye usimamizi wa miradi hiyo.
Ndejembi ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na wataalamu wa idara ya elimu wizarani hapo.
" Hatutamuelewa mtumishi yeyote ambaye hatosimamia fedha za miradi vizuri kwa maana hakuna (investment) iliyowahi kufanyika kama kipindi hiki cha Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na sisi ndio tupo kukamilisha historia hii na bado fedha zinaletwa. Niwatake kusimamia kwa weledi miradi hii ili watanzania waweze kunufaika nayo.
Tuhakikishe tunatoa huduma haraka pia kwa watumishi wetu hasa walimu ambao ndio jeshi letu kubwa tunalolitegemea, kama Rais wetu aliwajali kwa kuwapa promotion basi kwenye vitu ambavyo viko kwenye ngazi zetu tufanye na sisi kwa uweledi ili tumsaidie kazi Mhe Rais," Amesema Ndejembi.
Ndejembi pia amewataka wataalamu hao kujenga mahusiano mazuri na walimu ikiwemo kuwapatia motisha kwa wale wanaofanya vizuri ili kuwapa hamasa ya kufanya kazi kwa bidii zaidi.
Post A Comment: