NAIBU Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi na Mbunge wa Jimbo la Chamwino mkoani Dodoma, Deo Ndejembi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha Sh Milioni 125 kwa ajili ya ujenzi wa Hosteli za Shule ya Sekondari Zajilwa katika Kata ya Zajilwa huku yeye pia akiahidi kuchangia mifuko 200 ya Saruji za ujenzi wa Sekondari katika kijiji cha Chenene Kata ya Haneti.

Ndejembi ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kuzungumza na wananchi wa Jimbo hilo la Chamwino katika Kata mbili za Haneti na Zajilwa.

Akizungumza na wananchi wa Zajilwa, Ndejembi amesema Kata hiyo hapo mwanzo haikua na Sekondari lakini ndani ya kipindi kifupi cha Rais Samia kata hiyo imepata shule ya sekondari ambayo imegharimu kiasi cha Sh Milioni 470.

" Namshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ndani ya muda mfupi alitupatia Sh Milioni 470 ambazo zilituwezesha kufanikisha ujenzi wa Shule ya Sekondari hapa Zajilwa na sasa watoto wetu hawatembei tena umbali mrefu. Kama hiyo haitoshi hivi sasa ametupatia tena Sh Milioni 125 za ujenzi wa Hosteli.

Lakini pia Rais Samia ametupatia Sh Milioni 95 za ujenzi wa nyumba ya walimu katika Sekondari yetu hii. Haya ni mafanikio makubwa ambayo kata yetu imeyapata katika kipindi kifupi cha uongozi wake na tuna kila sababu ya kumshukuru na kumuunga mkono," Amesema Ndejembi.

Akiwa katika kata ya Haneti, Ndejembi amewataka wananchi wa kijiji cha Chenene kuandaa eneo ambalo litajengwa Shule ya Sekondari ambapo amewaahidi kuwa atapeleka mifuko 200 ya Saruji kama sehemu ya mchango wake kwa ajili ya kuanza ujenzi huo.

" Nafahamu watoto wetu hapa kijiji cha Chenene wanatembea umbali mrefu kwenda shule. Nimuagize Diwani kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji kuandaa eneo itakapojengwa sekondari hiyo na mimi kama Mbunge naahidi kutoa mifuko 200 ya kuanzia ujenzi huo na tutashirikiana pamoja hadi tukamilishe," Amesema Ndejembi.

Aidha amemtaka Meneja wa Tarura Wilaya ya Chamwino kufanya upembuzi yakinifu wa barabara ya Chenene-Itiso ili kuifungua barabara hiyo ya kiuchumi.

" Nimuagize pia Meneja wa Tarura Wilaya kufanya haraka upembuzi yakinifu wa barabara hii ya Chenene-Itiso ambayo itaunganisha kijiji hiki cha Chenene na Kata ya Itiso ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wetu ambao wengi ni wakulima kwa ajili ya kufanya biashara zao za mazao na kilimo," Amesema Ndejembi.

Share To:

Post A Comment: