Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai (kulia) akimuelekeza jambo Naibu ,Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, wakati wa ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John Jingu walipotembelea ofisi za Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara jana.
Na Mwandishi Wetu, Mtwara
NAIBU Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, amesema
ameridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na Bohari ya Dawa (MSD) hususani katika
utendaji na utekelezaji wa mikataba ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
nchini.
Dk. Mollel amesema hayo jana mkoani Mtwara katika
ziara ya kikazi akiwa ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. John
Jingu walipotembelea ofisi za Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara, kujionea hali ya
utoaji wa huduma na changamoto ya ufinyu wa ghala unaoikabili kanda hiyo.
Akizungumza na watumishi wa Kanda hiyo, Dk.
Mollel amesema, ameridhishwa na mabadiliko yanayofanywa na MSD hususani katika
utendaji na utekelezaji wa mikakati ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba
nchini.
Aliongeza kuwa hatua ya Serikali kuazimia
kuipatia MSD mtaji ni ya kujivunia, kwani itasaidia kuhakikisha MSD inatekeleza
mipango mikakati yake, ikiwemo ujenzi wa maghala na kuhakikisha dawa na vifaa
tiba vinapatikana nchini kote.
Sambaba na kutemebelea ofisi za Kanda hiyo,
Uongozi huo pia ulizuru eneo la Mikindani Mkoani Mtwara, ambalo lipo mkabala na
hospitali ya rufaa ya kanda ya kusini, mahali linapojengwa ghala jipya la
Bohari ya Dawa Kanda ya Mtwara na kujionea jinsi mchakato wa ujenzi wa ghala
hilo unavyoendelea.
Dk. Mollel ametumia fursa ya ziara hiyo,
kuwapongeza watumishi wa MSD Mtwara kwa juhudi na kujituma kwao katika
kuwahudumia wananchi licha ya changamoto ya udogo wa ghala uliopo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jingu,
amewataka watumishi hao kutobweteka na kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwani
serikali inaendelea kufanyia kazi changamoto zinazowakabili, ikiwemo tatizo la
ufinyu wa ghala hali inayosababisha ujenzi wa ghala jipya na la kisasa.
Ameongeza kuwa ziara yao katika Kanda hiyo, ni
kudhihirisha kwamba wanatambua changamoto iliyopo, hivyo kwa kushirikiana na
viongozi wengine wanaendelea kufanyia kazi changamoto hiyo, ili kupata tatuzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere
Tukai, amesema taasisi hiyo kupitia mpango mkakati wake, iko katika mchakato wa
maboresho ya huduma na utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na ujezi wa maghala
kwenye kanda tofauti nchini.
Amesema hatua hiyo itapanua wigo na uwezo wa MSD
katika kuwahudumia wateja wake kikamilifu, kwani itaongeza uwezo wa MSD
kuhifadhi bidhaa za kutosha kwaajili ya wateja na kupunguza gharama kubwa za
uendeshaji.
Mavere amezitaja Kanda hizo zitakazofikiwa na maboresho ya maghala kuwa ni pamoja na Mtwara, Mwanza, Kagera na Dodoma kwa kuanzia na baadaye kuangalia kanda nyingine zenye uhitaji.
Picha ya pamoja na viongozi wa MSD Kanda ya Mtwara.
Post A Comment: