Na Mwandishi Wetu -  MOI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. John Jingu kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu amepokea msaada wa vifaa tiba vya upasuaji kutoka Jumuiya ya St. Roch ya nchini Uingereza wenye thamani ya shilingi  bilioni 3.

Dkt. Jingu amepokea vifaa hivyo wakati alipotembelea Taasisi ya Mifupa ya MOI Katika hafla fupi na uzinduzi wa kambi ya siku nane ya matibabu iliyofanyika leo Septemba 21, 2023 katika Ukumbi wa MOI jijini Dar es Salaam.

Dkt. Jingu  ameishukuru Jumuiya ya St. Roch na Madaktari hao kwa msaada wa vifaa tiba na kuongeza kuwa utasaidia kuboresha huduma kwenye taasisi hiyo. 

Amesema vifaa hivyo vitatumika katika upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti, urekebishaji wa misuli ya magoti kwa njia ya matundu, urekebishaji wa ulemavu kwa watoto na upasuaji wa tishu (soft tissue surgery) pamoja na huduma nyingine za kibingwa.

“Msaada mlioutoa ni mkubwa sana, amesema Mkurugenzi Mtendaji wa MOI hapa kuwa msaada huu una thamani ya shilingi bilioni 3, hii si hela ndogo, msaada huu utasaidia kupunguza changamoto ya vifaa tiba vya upasuaji hapa MOI”. Alisema Dkt. Jingu.

Akizungumzia kambi ya matibabu Katibu Mkuu huyo alisema itasaidia kukuza ujuzi kwa madaktari wazawa na kwamba fursa hiyo italeta matokeo chanya katika utoaji tiba kwa wananchi.

“MOI hii baada ya siku nane, wageni wakiondoka haitakuwa MOI hii, kutakuwa na mabadiliko makubwa sana, hii ni fursa ya kila mmoja kujifunza, fursa hii itatoa matunda chanya na ya kudumu kwa jamii yetu”. Alisema Jingu. 

“MOI ni kituo cha umahiri sio tu kwa Tanzania lakini pia katika ukanda huu, unaenda kuimarisha pia ushirikiano baina ya Tanzania na Uingereza, matarajio yangu kwamba ushirikiano huu baina ya Taasisi yetu ya MOI na Jumuiya ya madaktari bingwa wa mifupa kutoka Uingereza utakuwa endelevu na wenye tija kawa manufaa ya watanzania wote”. Ameongeza Dkt Jingu. 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Prof. Abel Makubi ameishukuru Jumuiya ya St. Roch ya nchini Uingereza kwa msaada wa vifaa tiba vya upasuaji na kwamba vifaa na ujio wao utaleta matokeo chanya kwa MOI.

“Kwa niaba ya MOI nawashukuru, karibuni MOI hii ni hopsitali ya Taifa ya tiba ya mifupa, ubongo na ajali, tunatambua jitihada zetu katika kuasisi ushirikiano huu wa kudumu”. Amesema Prof. Makubi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameongeza kuwa msaada huo wenye thamani ya shilingi bilioni  3 utaongeza idadi ya wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji kwa siku kutoka wastani wa wagonjwa 24 hadi 42.









Share To:

Post A Comment: