Na John Walter-Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga ameweka jiwe la msingi katika shule mpya ya Awali na Msingi ya Queen Cuthbert Sendiga iliyopo kata ya Maisaka mjini Babati.

Ujenzi wa shule hiyo ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 380 za mradi wa BOOST, utasaidia kuondoa adha ya mrundikano wa wanafunzi darasani katika shule ya msingi Sinai.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la mmsingi katika shule hiyo Novemba 15,2013, Sendiga amesema shule hiyo imejengwa kwa ajili ya kuondoa msongamano darasani.

Aidha ameagiza madarasa yawekwe madawati ili watoto wanaosoma shule ya msingi Sinai waanze kuyatumia kuanzia jumatatu ijayo wakati suala la usajili wa shule mpya ukishughulikiwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Babati Abdulrahmani Kololi ambaye pia ndiye diwani wa kata ya Maisaka, amesema waliketi kikao na kukubaliana jina la shule iitwe jina la mkuu wa mkoa Queen Cuthbert Sendiga kama heshima kwake kwani alipoanza kazi  mkoani humo katika ziara yake ya kwanza aliondoa mvutano uliokuwepo kuwa shule ijengwe wapi na kufanikisha ujenzi huo kukamilika.  

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mjini Babati Elizabeth Marley amempongeza mkuu wa wilaya Lazaro Twange kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo wilayani humo.

Share To:

Post A Comment: