Kaimu Meneja Bohari ya Dawa (MSD) Mkoa wa Tabora Adonizedeck Tefurukwa, akizungumzia kuhusu hali ya ugonjwa wa malaria katika Mkoa wa Tabora katika kambi iliyowekwa na MSD kwa ajili ya kugawa vyandarua mkoani humo.
...................................................
Na Mwandishi Wetu, Tabora
MKOA wa
Tabora umetajwa kuwa wa kwanza kitaifa kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi
ya ugonjwa wa Malaria hali inayotokana na imani potofu ya matumizi ya vyandarua
vyenye dawa kuwa vinapunguza nguvu za kiume.
Akizungumza leo Septemba 25, 2023 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora Luis Bura
amesema hali ya ugonjwa wa Malaria ni mbaya na mkoa huo ndio unaongoza kwa
maambukizi ya ugonjwa huo.
Amesema takwimu zinaonyesha kiwango cha
maambukizi ya malaria kimeongezeka kutoka asilimia 11.7 mwaka 2016/2017 hadi
asilimia 23.4 mwaka 2022 wakati kiwango cha maambukizi ya malaria kitaifa ni
asilimia 8.1.
Hivyo kutokana na hali hiyo Serikali kupitia
Bohari ya Dawa (MSD) imetia kambi mkoani humo na kusambaza vyandarua vyenye
dawa.
“Tafiti zinaonyesha kiwango cha maambukizi ugonjwa
wa malaria kwa mwaka 2016/2017 kwa watoro wa umri wa miezi sita hadi miaka 5 ni
asilimia 20 na mwaka 2018 yameongezeka kufikia asilimia 23,” amesema.
Akizungumzia kiwango cha maambukizi ya ugonjwa
huo kitaifa ni asilimia 8.1 hivyo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 11.7 hali
inayosababisha mkoa huo kuongoza huku akieleza hali hiyo haikubaliki, hivyo ni lazima kuwa na nguvu ya pamoja kwa
watendaji na jamii kuhakikisha maambukizi hayo yanapungua.
Amefafanua kuwa
makundi ambayo yako hatarini ndio yatanufaika na vyandurua hivyo
wakiwemo watoto chini ya miezi tisa na miaka mitano, wajawazito, wanafunzi ,
wazee wa miaka 60 na watu wanaoishi na VVU.
Ameongeza kuwa
kaya zaidi ya 300,000 kati ya kaya 400,000 ambazo zitapewa vyandarua
hivyo ambavyo ni zaidi ya milioni 1.8.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa MSD Tabora
Adonizedeck Tefurukwa, ameushukuru uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa
kuendelea kuboresha huduma za afya nchini na kuwahakikishia wananchi wa Tabora
kuwa, kila mnufaika wa vyandarua hivyo atafikiwa.
Amesema katika usambazaji huo wamejipanga
ipasavyo na wanatimu ya kutosha kufika katika kila maeneo na ili kufanikisha
hatua hiyo, wamekodisha maghala mawili ya ziada eneo la Nzega na Igunga.
Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Honoratha Rutatinisibwa amesema takwimu hizo zinatokana na mkoa huo wananchi wake kuwa na imani potufu ya matumizi ya vyandarua vyenye dawa kuwa vinapunguza nguvu za kiume.
Post A Comment: