Na Dotto Mwaibale, Lindi
MKAZI wa Kijiji cha Milola kilichopo Kata ya Milola mkoani Lindi, Esha
Selemani Peleu }35 } maisha yake yapo hatarini kutokana na moyo wake kuwa na
tundu na ameshindwa kupata matibabu kwa sababu hana fedha.
Akizungumza na waandishi wa habari, Esha amesema alianza kuwa na changamoto
ya maradhi hayo mwaka 2020 ambapo alikwenda Hospitali ya Misheni ya Ndanda na
baada ya kufanyiwa vipimo moyo wake uligundulika kuwa na tundu.
Amesema daktari aliyemuhudumia alimuandikia dawa ambazo hazikumbuki kwani
vyeti vyake vilipotea lakini vilikuwa ni vidonge vidogo vyeupe ambavyo
alielekezwa avikate mara nne na avitumie kutwa mara moja na kuwa gharama ya
vipimo na hizo dawa ilikuwa ni zaidi ya Sh.60,000.
Alisema fedha hizo alipewa na mume wake ambaye ametengana naye baada ya kupata changamoto
hiyo na kuwa sasa anaishi na mtoto wake kwa wazazi wake ambao hawana uwezo na
tangu apate matibabu hayo huu ni mwaka wa tatu anaishi kwa mateso na hana raha
ya maisha kutokana na maumivu makali anayoyapata.
'' Naishi kwa mashaka kifua kinabana, napumua kwa shida nikienda kuchota
maji napata maumivu makali wakati wa kupumua nalazimika kuvuta pumzi
kidogokidogo ndipo napata nafuu haya ndiyo maisha yangu ya kila siku na siwezi
kukaa tu nyumbani pasipo kufanya kazi naomba msaada wenu mwenzenu nakuja
jameni,'' alisema Esha.
Anasema changamoto hiyo ilimuanza wakati anajiandaa kulala alipata mshituko
wa moyo na akapoteza kumbukumbu tangu wakati huo mwili wake umekuwa ukidhohofu
na kumfanya asijue cha kufanya hivyo anamuomba Waziri wa Afya Ummy Mwalimu na
wadau wengine mbalimbali wamsaidie kupata matibabu kwani wakati mwingine hata
kula yake na mwanaye huyo aliyemtaja kwa jina moja la Rumaydha imekuwa ya
changamoto kutokana na mazingira anayoishi ya kutokuwa na fedha ya kujikimu.
Taasisi na mtu yeyote ambaye ataguswa kumsaidia dada yetu huyu ambaye anapitia katika wakati mgumu kutokana na maradhi hayo yanayomsumbua na kushindwa kufanya kazi yoyote ambayo inaweza kumpatia kipato na kupata matibabu anaweza kuwasiliana naye moja kwa moja kwa namba ya simu 0785 192412 au namba 0754362990 na Mungu atakubariki kwani kutoa sio mpaka uwe na fedha nyingi hata hiyo Sh.2000 yako kwake itamtosha.
Post A Comment: