Chanthaburi-Thailand


Serikali katika Mji Mkongwe na Maarufu kwenye shughuli na Biashara ya Madini ya Vito wa Chanthaburi nchini Thailand umeiomba Tanzania kuufungulia milango na kuimarisha ushirikiano kwenye uendelezaji wa Sekta  Ndogo  ya Madini ya Vito.

 Wito huo unafuatia ziara ya Ujumbe wa Tanzania katika mji huo Septemba 11,  2023 ambao ulipata fursa ya kutembelea viwanda vidogo vya kuongeza thamani madini kuanzia kuchoma ili kuongeza ubora na kusanifu madini ili kutengeneza bidhaa za urembo za usonara. 

Ujumbe huo ulitembelea soko kubwa la madini ya vito vya thamani ambalo pia limeweka makumbusho ya madini ya vito vya thamani vya aina mbalimbali vinavyozalishwa kutoka nchi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania. Katika sehemu ya makumbusho madini ya vito ya aina mbalimbali yameelezwa umuhimu wake na hivyo kuifanya kuwa pia sehemu ya mafunzo na matangazo ya kuhamasisha biashara.

Biashara ya madini na shughuli za uongezaji thamani madini katika Mji wa Chanthaburi kwa kiasi kikubwa unategemea malighafi za madini kutoka Tanzania, Nigeria, Madagasca na Msumbiji. Aidha, madini ya Sapphire na Rubi ya Mundarara Wilayani Longido Mkoa wa Arusha ni miongoni mwa madini maarufu katika mji huo.

Aidha, Septemba 12, 2023, akizungumza baada ya kikao na Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Biashara katika mji wa Chanthaburi nchini humo Bw. Jirawuth Suwanna-arji,  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amesema Mkurugenzi huyo ameiomba Tanzania kuifungulia milango ya ushirikiano wa kibiashara na mji huo kutokana na ujuzi, maarifa waliyonayo katika eneo la uongezaji thamani madini  ili kurithisha maarifa hayo kwa Watanzania ikiwemo kufanya biashara  na shughuli za uongezaji thamani madini kwa kushirikiana.

 Ameongeza kuwa, Mkurugenzi huyo ameeleza wazi kuwa anafahamu kwamba nchi ya Tanzania inayo madini mengi ya vito vya thamani ambavyo kwa kiasi kikubwa vimekuwa vikitumiwa na wafanyabiashara katika mji huo na hivyo kueleza kwamba, ushirikiano huo utakuwa wa manufaa  kwa pande zote mbili na  kwamba, ameikaribisha Tanzania kupeleka wataalam wake kujifunza  shughuli za uongezaji thamani madini  ili kupata ujuzi unaohitajika katika soko la dunia.

 ‘’Ni ushirikiano ambao tumeufungua na tunauimarisha, sehemu hii ya biashara ya vito inaweza kuimarisha ushirikiano wetu na si tu katika madini bali pia katika shughuli nyingine,’’ amesisitiza Mbibo.

Aidha, katika mazungumzo yake na Wizara, Mkurugenzi huyo amewakaribisha wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kushiriki katika Maonesho ya Vito katika mji huo yayakayofanyika kwa awamu  tarehe 12 -31  Oktoba, 2023.

“Kwa kuwa tarehe za maonesho hayo zinaingiliana kwa kiasi kikubwa na Jukwaa letu la Kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini litakalofanyika tarehe 25 na 26 Oktoba, 2023, tumewaomba na wao wachache waje kushiriki jukwaa letu na sisi wachache watakaoweza waende kwao,’’ amesema Mbibo.

 Akizungumza baada ya kutembelea viwanda vidogo vya kuongeza thamani madini ya Sapphire,  Kamishna Msaidizi  Sehemu ya Uongezaji Thamani Madini Wizara ya Madini Bertha Luzabiko amesema hiyo ni teknolojia ambayo ina fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuongeza thamani madini yao kwa kuongeza ubora kwa njia ya kuchoma  katika nyuzi joto kubwa na hivyo kuyafanya madini yao kuwa na bei kubwa sokoni. 

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali wakiwemo wanafunzi na wafanyabiashara kupata fursa ya kujifunza zaidi teknolojia hiyo ili iweze kuja kutumika nchini na kuchochea shughuli za uchumi kupitia madini hayo ya vito yakiwemo sapphire, rubi na mengine.

 Aidha, Bertha ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wenye viwanda vidogo kujifunza teknolojia hiyo kuwezesha upatikanji wa vifaa hivyo kutokana na wingi wa rasilimali madini ya vito yanayopatikana nchini.



Share To:

Post A Comment: