MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, ameshiriki mahafali ya darasa la saba ya Shule ya Msingi Mahambe na kukabidhi madawati 44 yenye thamani ya Shilingi Milioni 2.8 ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa samani shuleni hapo.
Mbali na madawati hayo pia amechangia Shilingi 500,000 ya kununua sinki la choo kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ,Shilingi 200,000 ya ufundi,gunia moja la mchele,sukari,jiko la gesi kwa ajili ya chai ya walimu asubuhi kama motisha na mipira miwili ya kuchezea wanafunzi netball na football.
Mh Mtaturu ametoa misaada hiyo kufuatia risala ya shule iliyosomwa na mwalimu Issa Omary.
“Maendeleo ya ufaulu ni mazuri ,lakini pamoja na mafanikio haya tunazo changamoto zinazowakabili wanafunzi na hivyo kuathiri maendeleo ya shule yetu,shule yetu inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu ya shule,madarasa,nyumba za walimu na matundu ya vyoo,”ameeleza.
Amesema kama shule kwa kushirikiana na wazazi na wadau mbalimbali wamefanikiwa kutatua baadhi ya changamoto hizo kwa kuanzisha ujenzi wa matundu saba ya vyoo na sasa wapo hatua ya upigaji lipu na kuweka milango na masinki.
Amesema serikali kuu imewapeleka Shilingi Milioni 40 ili kujenga madarasa mawili na ofisi ujenzi ambao upo hatua ya Msingi.
Akikabidhi misaada hiyo Mtaturu amesema tangu anaingia bungeni aliweka bayana kuwa elimu ni kipaumbele chake cha kwanza na ndio maana amekuwa akijaribu kushirikiana na serikali kutatua changamoto zilizopo katika sekta hiyo.
“Niwapongeze sana kwa hatua mliyopiga ya kushiriki shughuli za maendeleo kwani maendeleo ni ya wananchi wenyewe,serikali inafanya kwa upande wake na jamii inao wajibu wa kushiriki kwenye miradi ya maendeleo ili kuimiliki na kuitunza,”amesema.
Amesema kazi ya kuhamasisha wanachi kushiriki shughuli za maendeleo aliianza mwaka 2016 na anafurahi kuona wananchi wameamua kuunga mkono serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kinyume cha maneno ya awali kuwa serikali itafanya peke yake.
“Nimefurahi zaidi mmeweza kuchanga nafaka magunia 20 kwa ajili ya lishe shuleni,name nimewachangia mchele,sukari na gesi,niwaombe tuendelee kuiunga mkono serikali yetu ,”ameongeza.
Mtaturu amewahakikishia wananchi kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia ili kuongeza ubora wa elimu na ufaulu sambamba na kuongeza idadi ya walimu kwenye shule zote.
Akiwa shuleni hapo Mtaturu amekagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa mawili na ofisi katika shule ya Mahambe ambayo serikali imepeleka fedha Shilingi Milioni 40.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wananchi Diwani wa Kata ya Unyahati Abelly Suri amemshukuru Mbunge kwa kuendelea kuwa bega kwa bega na wananchi wakati wote.
“Mbunge umekuwa sauti yetu Bungeni kila mara tunakusikia ukitusemea,hata madarasa haya mawili tuliyoletewa ni matokeo ya kazi yako njema ya kutuombea fedha za miradi,tunaomba utufikishie shukrani zetu kwa Rais Samia kwani tunaona jitihada anazofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo,”amesema.
Amesema wao Kata ya Unyahati ni mashahidi ,wamepokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikimemo Shilingi Milioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule ya Msingi Matare.
“Tumepokea pia Shilingi Milioni 967 za ujenzi wa madarasa na bweni katika shule ya sekondari ya Unyahati na Shilingi Milioni 258 kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa maji kijiji cha Matare,hizi ni fedha nyingi zimetolewa na shukrani zetu ni kuzidi kumuombea awe na afya njema ya kuwatumikia watanzania,”ameshukuru.
Shule hiyo ilianzishwa mwaka 1979 na ina wanafunzi 467 walimu 8.
Post A Comment: