Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amehimiza uwepo wa mashindano ya michezo mbali mbali, ili kujenga ustawi bora wa vijana, jamii na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Othman amehimiza hayo leo katika Fainali ya Mpira wa Miguu, ya Coco Sports Cup, iliyochezwa katika Viwanja vya Mao Tse Dong, Mkoa wa Mjini- Magharib, Unguja.
Amesema kuwa pamoja na kusaidia kujenga na kurejesha hamasa Nchini, mashindano hayo yanawapatia mbadala wa kazi za kujishughulisha vijana maishani, na hivyo kusaidia ustawi bora katika jamii.
"Pamoja na kurejesha hamasa, mashindano yaaina hii yanawapa fursa ya kazi mbadala vijana wetu, na pia kuwaepusha na majanga mbali mbali yakiwemo matumizi ya dawa za kulevya", amesema Mheshimiwa Othman.
Akiongelea suala la kukosa na kushuka hamasa michezoni, Mheshimiwa Othman amesema inabidi mamlaka ziketi na kujitathmini kwa kuangalia lilipo tatizo, kwani ushabiki unaojitokeza katika Mashindano ya 'Ndondo" ni ithibati kwamba " mchezo wa mpira wa miguu bado una wenyewe na unaendelea kupendwa hapa Visiwani".
Aidha Mheshimiwa Othman ameahidi kwamba Serikali inao wajibu wa kuungamkono juhudi zinazochukuliwa na waandaaji wa mashindano mbali mbali ili kusaidia kuibua na kukuza vipaji.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Mhe. Rashid Simai Msaraka, amewahimiza vijana kuitumia michezo kama fursa muhimu ya kujiendeleza kwaajili ya maisha yao ya sasa na baadae.
Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar, Bw. Ameir Makame, amesema pamoja na changamoto ziliopo, Serikali haitosita kusaidia kwa kila inavyowezekana ili kuinua ushiriki wa vijana na kuimarisha Sekta hiyo kwaajili ya maendeleo.
Fainali hiyo imemalizika kwa Timu ya Ubinaadamu Kazi kutoka Jang'ombe kuibuka Washindi wa Mikwaju ya Penalti 4-3 dhidi ya Miembeni, baada Mchezo kuisha kwa Suluhu ya Bila Kufungana katika Muda wa Kawaida.
Mshindi amejinyakulia Kikombe na Kitita cha Shilingi Milioni 12 na Medali, dhidi ya Milioni 6 za Mshindi wa Pili.
Fainali hiyo imewajumuisha umati wa washabiki wa michezo na Viongozi mbali mbali wa Serikali na Vyama vya Siasa, wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania, Mhe. Hamad Masauni, na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar, Mhe. Salim Bimani.
Mashindano hayo yamedhaniwa na Kituo cha Habari cha Coconut, sambamba na Wafadhili mbali mbali akiwemo Mmiliki wa Vyombo vya Habari Nchini, Bw. Ali Dai.
Post A Comment: