Viongozi wa Kampuni ya Qwihaya General Enterprises LTD inayojihusisha na biashara ya mbao wakikabidhi msaada wa mbao 2200 kwa kaya 50 za mitaa ya Buganda na Ilemela Mahakamani katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ambazo nyumba zao zilibomolewa na mvua Septemba 6 mwaka huu.
.....................................................
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
KAMPUNI ya Qwihaya General Enterprises LTD
inayojihusisha na biashara ya mbao imetoa msaada wa mbao 2200 kwa kaya 50 za
mitaa ya Buganda na Ilemela Mahakamani katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza
ambazo nyumba zao zilibomolewa na mvua Septemba 6 mwaka huu.
Kaya hizo zenye jumla ya wakazi 350 zimepewa msaada huo wa mbao kwa ajili ya
kupaulia upya nyumba zao.
Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni
13.2 umekabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Benedicto Mahenda
Qwihaya kwa wakazi hao ikiwa ni kuitikia wito wa Serikali kwa wadau kujitokeza
kusaidia waathirika wa janga hilo.
Kupitia msaada huo, kaya 16 za Mtaa wa Buganda
ambao nyumba zao zilibomoka kabisa zimepata vipande 47 vya mbao huku kaya
nyingine 13 ambazo nyumba zao hazikupata madhara makubwa zikipewa mbao 30 kila
moja.
Msaada kama huo pia umetolewa kwa Kaya 21 kutoka
Mtaa wa Ilemela Mahakamani ambao pia waliathiriwa na mvua hizo zilizowaacha
wananchi wakilala nje kwa kukosa makazi.
Akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Qwihaya, Benedicto
Mahenda amesema uongozi wa kampuni hiyo inayojihusisha na biashara ya mazao ya
misitu uliguswa na taarifa za janga hilo zilizotangazwa kupitia vyombo vya
habari ikiwaonyesha watoto, wazee na wanawake wakiwa wamelala nje kwa kukosa
makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.
“Tumetoa sehemu kidogo ya tulichojaaliwa na
Mwenyezi Mungu kusaidia waathirika kujenga upya makazi yao,’’ amesema Mahenda.
Akishukuru kwa niaba ya wenzake, Regina Chrisant,
mmoja wa waathirika, mkazi wa Mtaa wa Buganda ameishukuru kampuni ya Qwihaya,
Serikali na wadau wote kwa misaada inayowawezesha kurejea katika maisha yao ya
kawaida baada ya janga lililowaacha wakiwa hawana makazi.
‘’Misaada hii ya hali na mali imeturejeshea
matumaini siyo kwa kwa kutuwezesha kuyajenga upya makazi yetu, bali pia
inaonyesha jinsi Watanzania tunavyoishi kwa upendo miongoni mwetu,’’ amesema
Regina.
Stanslaus Francis, mwathirika mwingine aliyepokea
msaada ameomba wadau zaidi kujitokeza kusaidia waathirika kurejea katika maisha
yao ya kawaida baada ya janga hilo ambalo alikusababisha majeruhi wala vifo.
Shukrani zingine zimetolewa na Diwani wa Kata za
Shibula iliko Mtaa wa Buganda, Swila Dede (CCM) huku akiwaomba wadau wengine
kujitokeza kuitikia wito wa Serikali wa kusaidia wananchi kwa sababu bado kuna
mahitaji mengi ikiwemo ya chakula, samani za ndani na vifaa vingine vya ujenzi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buganda,
Evarsit Chikanga amewataka wanaopokea msaada kuitumia kwa malengo mahusui
ikiwemo kujenga upya makazi yao huku Mratibu wa Maafa Manispaa ya Ilemela,
Jamses Wembe akiwataka wananchi wanaoishi jirani na fukwe na wanaofanya
shughuli za kiuchumi na kijamii ndani ya Ziwa Victoria kuchukua tahadhari mvua
na upepo mkali.
Kwa mujibu wa Wembe, tahadhari hiyo inatokana na utabiri iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu uwezekano wa ukanda wa Ziwa Victoria kupata mvua nyingi utakaoambatana na upepo mkali ndani ya siku tano zijazo.
Post A Comment: