Na Immanuel Msumba ; Namanga

Mazingira maana yake ni jumla ya vitu vyote vinavyomzunguka binadamu pamoja na yeye mwenyewe, viumbe vyenye uhai na visivyo na uhai, vya asili na visivyo vya asili na jinsi vinavyotegemeana. Mazingira ni ghala la kuhifadhi malighafi zote zinazohitajika kuendeleza uhai wa viumbe hai na mfumo-ikolojia.

Binadamu ni sehemu ndogo sana ya mazingira. Mahitaji yote ya binadamu hutunzwa ndani ya mazingira. Mazingira yanahusisha maumbile halisi yawazungukayo binadamu ikiwa ni pamoja na hewa, ardhi, maji, tabianchi, sauti, mwanga, harufu, ladha, vijiumbe, hali za kibiolojia za wanyama na mimea, rasilimali za kitamaduni na masuala ya uchumi jamii na inahusisha mazingira asilia na yaliyoundwa na binadamu na jinsi yanavyoingiliana.

Mazingira safi ni kitovu cha afya bora na maendeleo kwa wananchi. Ili kufikia lengo la kuwa na mazingira safi, ni lazima kuwa na mikakati endelevu ya kudhibiti uchafuzi wa makazi kutokana na taka zinazozalishwa kila siku.

Ili kuweka usimamizi endelevu wa usafi katika makazi ni lazima kuweka misingi ya usimamizi, tathmini na kuchukua hadhari kuhusu madhara kwa mazingira, kwa kudhibiti taka kuanzia zinapozalishwa, ukusanyaji, usafirishaji na utupwaji wake.

Katika Kata ya Namanga Wilayani Longido mpakani mwa Tanzania na Nchi ya Kenya wananchi wanaoishi kwenye mji huo wameiomba Serikali kuhamisha dampo lililopo katika mji huo kutokana na kero kubwa ya moshi na harufu inayozuka katika dampo hilo wanayoipata wakiwa kwenye biashara zao na majumbani mwao.

Joseph Loah Laizer ambaye ni dereva bodaboda  katika mji huu ametueleza kwamba eneo lililotengwa kwa ajili ya dampo limekuwa sana karibu na makazi yao hali ambayo inaweza kusababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

“Dampo hili linahatarisha usalama wa afya za wakazi wa hapa namanga kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa utupaji wa taka,haiwezekani taka zimwagwe pembezoni mwabarabara ambayo inatumiwa na wakazi wengi wa hapa na wanaosafiri Kwenda nchi ya Jirani ya kenya, walianzisha dampo kule kimokouwa lakini wameshindwa kulisimamia na kule lazima upeleke na gari kwani ni mbali,tunaiomba halmashauri itangaze tenda kwa mkandarasi ili takataka zizolewe kupitia mkandarasi ili ziweze Kwenda kutupwa huko nje ya mji”

Hata hivyo Bi. Namnyaki Mollel ambaye ni mmachinga katika mpaka wa Kenya na Tanzania amesema kumewepo na usumbufu mkubwa wa harufu na moshi mkubwa wakati wa uchomaji takataka katika dampo hilo jambo ambalo limekuwa likiwaadhiri wasafiri Pamoja na wafanyabiashara wanaozuka mji huo.

“Moshi mkali unatuadhiri pindi wanapokuwa  wanapochoma taka kwenye dampo pale mtoni na unatuadhiri kiafya na kusababisha vikohozi kwa watu ambao tunafanya biashara karibu na eneo hili” Alisema

Aidha Namyaki alienda mbali na kuulalamikia uongozi wa halmasahauri kitengo cha usafi na mazingira kwa kusema kuwa wameshidwa kutekeleza na kuendana na kauli ya Serikali ya Awamu ya sita ya kuwataka wanachi kufanya usafi ili kuweza kujikinga na magonjwa yanayoweza kusababishwa na uchafu.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Namanga Hassan Ngoma amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kueleza kuwa kwa sasa huduma ya dampo walilokuwa wanalitumia hawalitumii kutokana na kushindwa kumlipa mkandarasi ila sasa wanahangaika wenyewe kama wananchi baada ya kujaza takataka majumbani huwa wanatumia bodaboda na pikipiki za matairi matatu {Virikuu} kwenda kutupa takataka katika mto ambao unatiririsha maji kwenye vijiji ya jirani vya jamii ya kifugaji.

"Kwa sasa wananchi wa Namanga wanamwaga takataka pale darajani hapo karibu na katoliki,muda huu hatuna gharama rasmi mtu anajaza takataka zake analipia elfu 1000 usafiri unashushiwa hapo mtoni maisha yanaenda,ila kwa upande wa maji taka bwana afya anafanya mpango kwa watu wote wanaotaka kuvutiwa kisha anaagiza gari kutoka Arusha ndipo linavuta linapeleka kule kwenye dampo la kimokowa"

"Sisi kama Kata tulishafunga kumwaga takataka pale darajani kwani hapa tunakituo kikubwa cha forodha {one stop border} kinazalisha uchafu mwingi ndio maana tulilazimika kutafuta mkandarasi ili takataka hizi ziwe zinatupwa kule kimokowa kwenye lile eneo ambalo lilitengwa."

"Athari zipo nyingi sana pale pembeni kuna mto tunapomwaga takataka hizi na maji ya mvua yanapotiririka pale yanakwenda kwenye jamii ya wafugaji ambapo kule kuna mifugo ambapo ukienda uchafu kule ngombe watakunywa na wakishakamuliwa maziwa yataletwa kwetu ndipo tutakunywa uchafu na kupata magonjwa ya mlipuko."

"Tumeshwindana na mkandarasi kutokana na gharama za uendeshaji kwani mapato hayakuwa mazuri sana hivyo tunaiomba Halmashauri kuangalia namna bora kusaidia mji huu wa Namanga." Aliongeza

Ikumbukwe Mwaka jana katika viwanja vya Nyerere Square jijiniDodoma wakati Makamu wa Rais wa Jamhuri yaMuungano wa Tanzania Dkt.Philip Mpango akizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, uzinduzi uliofanyika Makamu wa Rais alisema kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu,upandaji miti, kupendezesha miji, kufanya kusafi katika maeneo yote ya makazi na biashara, viwandani na masokoni ni lazima kuanzia sasa kuwa kazi za kudumu.

Aidha, alisema kuwa viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wanapaswa kusimamia uhifadhi wa mazingira na suala hilo litakuwa kipimo cha utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema ni muhimu kuondoa nadharia katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuwa na mipango isiotekelezwa bali inahitajika kazi ya ziada itakayotoa matokeo chanya katika kuhifadhi mazingira. Alisema sheria ndogondogo za uhifadhi wa mazingira zinapaswa kusimamiwa ikiwemo faini na ikiwezekana kuongeza faini hizo ili kukomesha waharibifu wa mazingira.

Alisisitiza kuwa zoezi la kutunza mazingira ni lazima kuwa shirikishi kwa wadau wote kuanzia mijini na vijijini na kuagiza wizara na taasisi zote za serikali kuhakikisha wanapanda miti.

Licha ya maagizo hayo ya Makamu wa Rais hali ni tofauti kwa wilaya ya Monduli ambapo imeshindwa kujenga dampo la kutupa taka licha ya kutengwa eneo katika kata ya Meserani.

Uwepo wa dampo hilo katika makazi ya watu limekuwa hatarishi kwa afya zao haswa watoto kutokana na watoto wengi kwenda kucheza kwenye eneo hilo ambalo halmashauri imeshindwa hata kuweka uzio kwa ajili ya kudhibiti watoto kuingia katika eneo hilo hatarishi.

Aidha taka hizo zimekuwa zikisambazwa na mbwa hadi kwenye makazi ya watu hali ambayo itishia usalama wa afya za wananchi huku baadhi wakiwa na hofu ya kupatwa na magonjwa ya mlipuko.

Je nini kifanyike?

1. Uhamishaji wa Dampo: Serikali ifanye tathmini ya kina kuhusu dampo la kisasa na kutafuta eneo lingine mbali kidogo na makazi ya watu ili kuhamishia dampo hilo.

2. Uboreshaji wa Usimamizi wa Taka: Serikali iweke mkakati wa usimamizi wa taka ambao utajumuisha ukusanyaji wa taka, usafirishaji, na utupaji kwa njia endelevu.

3. Elimu kwa Umma: Wizara ya Afya na Mazingira ifanye kampeni za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira, madhara ya uchafuzi wa mazingira, na jinsi ya kutupatupa taka kwa njia inayofaa.

4. Teknolojia Safi: Kutumia teknolojia safi na za kisasa katika kusimamia na kutupa taka. Kwa mfano, teknolojia za kugeuza taka kuwa nishati au mbolea zinaweza kutumika.

5. Ushirikishwaji wa Jamii: Wananchi wa Namanga wawe sehemu ya suluhisho kwa kushirikishwa katika michakato ya maamuzi, utunzaji wa mazingira, na utekelezaji wa miradi inayohusiana na usafi wa mazingira.

6. Usimamizi Thabiti: Kuwepo na sheria kali na wazi kuhusu utupaji wa taka, na kuhakikisha kuwa sheria hizo zinatekelezwa kikamilifu.

7. Uwezeshaji wa Asasi za Kiraia: Asasi za kiraia, vikundi vya jamii, na taasisi zisizo za kiserikali zinaweza kusaidia katika kuendesha kampeni za usafi na kusimamia utekelezaji wa sera za mazingira.


8. Mikakati ya Kifedha: Serikali na wafadhili wanaweza kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utupaji taka na kufadhili teknolojia safi.

9. Ufuatiliaji na Tathmini: Kuweka mfumo wa kufuatilia na kutathmini hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha kuwa zinafaa na zinaleta mabadiliko yanayotarajiwa.

10. Ushirikiano wa Kikanda: Kwa kuwa Namanga iko kwenye mpaka wa Tanzania na Kenya, nchi zote mbili zinaweza kushirikiana katika kutatua tatizo hilo kwa manufaa ya wakazi wote wa eneo hilo.

Hatua hizi, zikitekelezwa kwa dhati na ushirikiano wa dhati kutoka kwa wadau wote,

zinaweza kusaidia kutatua tatizo la uchafuzi wa mazingira katika Kata ya Namanga.

Share To:

Post A Comment: