Na John Walter-Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Naibu waziri wa Katiba na sheria Paulina Gekul, amekabidhi msaada wa mitungi 200 kwa mama na baba lishe wa Mji wa Babati.
Hatua hiyo ni kuunga mkono maagizo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuitaka jamii kutumia nishati mbadala ili kulinda mazingira na kuepuka mabadiliko ya tabia ya nchi.
Akikabidhi mitungi hiyo iliyotolewa na Kampuni ya Orxy, Gekul amesema serikali chini ya Rais Dk. Samia, inathamini wananchi wake na itasimamia kikamilifu kuhakikisha wanatumia nishati hiyo mbadala na kuokoa misitu.
Ameeleza, matumizi ya gesi hiyo yatasaidia ufanisi kwa baba na mama lishe hao, kulinda mazingira na kujiepusha na matumizi ya mkaa.
Ameishukuru Kampuni ya Orxy kwa kutoa mitungi hiyo bure na kuwaomba mama na baba lishe hao, kutumia bidhaa za kampuni hiyo ya wazawa.
Aidha amewataka wajasiriamali wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa uhuru kwa kuwa serikali inawapenda na kuwajali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Babati Abdulrahmani Kololi amemsifu Mbunge kwa hatua hiyo.
Wakizungumza baada ya kupokea mitungi hiyo Happy Massawe na Rosemarry Maswi, wamesema gesi hizo zitawasaidia kuokoa Muda na kutoa huduma ya chakula kikiwa cha moto muda wote haswa katika wakati huu ambao wanajiandaa kuwahudumia Watanzania wengi watakaowasili mjini hapa kwa ajili ya shughuli tatu Kubwa za Kitaifa ikiwemo wiki ya vijana Kitaifa, kumbukizi ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru Oktoba 14 2023.
Post A Comment: