Angela Msimbira,KONDOA
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshungulikia Elimu, Dkt.Charles Msonde amesema mwalimu ni mwezeshaji wa ujuzi ndani ya jamii hivyo wanawajibu wa kuhakikisha wanafundisha kwa umahiri.
Akifungua Septemba 29, 2023 mafunzo ya uongozi na usimamizi wa shule kwa walimu, Wakuu wa shule za msingi yaliyofanyika katika Halmashauri ya Mji Kondoa, amesema mwalimu ni kiungo muhimu katika kuboresha elimu nchini na kuwahimiza kutimiza kikamilifu majukumu yao.
"Walimu wamepewa dhamana kubwa ya kuboresha elimu katika taifa letu la Tanzania kwa kuwa ndio anayeleta elimu bora katika taifa lake hivyo tunahitaji miundombinu, vifaa vya kufundishia lakini ukimchukua mwalimu bora ambaye ufundishaji unatoka kwenye moyo wake kwa ajili ya kusaidia watoto wa taifa lake hata akikaa kwenye mti akafundisha wanafunzi wataelewa,"amesema.
Amesema katika uwajibikaji wa mwalimu bora katika shule ni uwepo wa Mwalimu mkuu bora mwenye maono ya kuleta mabadiliko katika shule yake na taifa kwa ujumla.
Amebainisha kuwa walimu wanajukumu kubwa la kumjenga mtoto katika maadili na ni wajibu wa walimu na maafisa maendeleo ya jamii kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa malezi ya watoto ili watoto waepukane na ukatili wa kijinsia.
"Hivyo mwalimu ni mlezi wa watoto kwa kuhakikisha wanapata ujuzi, umahiri, stadi na mwelekeo wa kuwawezesha watoto hao kujiletea maendeleo yao binafsi, jamii na Taifa kwa ujumla, "amesema.
Ameeleza kuwa serikali imeandaa sera , mitaala na miongozo mbalimbali ni jukumu la Mwalimu kuhakikisha anaisimamia kwa kuwa na watoto wenye umahiri, ujuzi na uelewa wanapatikana ndani ya jamii.
Aidha, amesema kuwa mwalimu akisimama katika nafasi yake ipasavyo kwa kuhakikisha kila ngazi ya darasa kuna mabadiliko itasaidia kuleta mapinduzi ya elimu nchini
Post A Comment: