ALIYEKUWA diwani wa Kata ya Mkuzi iliyopo wilayani Muheza mkoani Tanga kwa tiketi ya CHADEMA George Chambai amejiuzulu nafasi yake hiyo na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kutokana na uwamuzi wake huo, sasa ni rasmi kata 245 zilizopo katika majimbo 12 Mkoa wa Tanga yatakuwa ya CCM kama ambavyo Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Rajabu Abrahamani alivyoahidi kuzirejesha kata saba zilizokuwa upinzani mkoani hapa.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika viwanja vya Sokoni Mkuzi, diwani huyo amesema ametekeleza takwa lake la kikatiba kuhama chama cheke cha awali na kujiunga na CCM.

Amesema hakushawishiwa na mtu yeyote katika uwamuzi wake, bali amefanya  hivyo baada ya kuridhishwa na kasi ya maendeleo inayofanywa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan lakini na ubora wa  wenyekiti wa CCM wa mkoa wa Tanga Ustadh Rajabu.

"Naomba nisieleweke vibaya hili ni takwa la kikatiba, mtu kuhama chama na kujiunga na Chama kingine, lakini pia nimetumia hesabu, kama Rais anafanya kazi kubwa kuleta maendeleo mimi nang'ang'ana nini kwenye chama kisichokuwa na Ilani?

"Nimehama CHADEMA  kwa mapenzi yangu, siasa siyo chuki wala ugomvi, tunataka watu wapate maendeleo na nawapenda sana watu wa Mkuzi.Wanajua  Rais wao anafanya mambo mengi kwenye Kata hii, hivyo sikuwa na sababu ya kubaki upinzani."

Diwani huyo baada ya kurejea CCM alitoa kero zake nne zilizopo katika kata hiyo ambazo ni kukosekana kwa umeme katika kitongoji cha Sakadange, ujenzi wa hule mpya msingi Lunguza.

Pia amezungumzia  fidia ya wananchi wa Mkuzi walitoa eneo lao kupisha ujenzi wa Kituo Cha Afya na kumalizwa kwa kituo hicho ambapo Mbunge wa Jimbo hilo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA na Mwenyekiti wa Chama walimuahidi kero hizo zitatatuliwa.

Kwa upande wake MwanaFA ambaye pia ni Naibu Waziri wa Utamaduni , Sanaa na Michezo amemuhakikishia kuwa kwa amerudi CCM kero hizo wataanza kuzifanyia kazi haraka kwasababu amekuwa mwenzao.

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa CCM aliwaeleza wananchi ametekeleza ahadi yake kwamba ukichaguliwa kuwa Mwenyekiti katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana atahakikisha madiwani wote saba waliokuwa CHADEMA wanajiunga na CCM.

"Nimemsikia Mbowe (Freeman Mwenyekiti wa CHADEMA) amemchukua Mwenyekiti wa Kijiji kule Lushoto, CCM imemsimamisha kwa utovu wa nidhamu wakamchukua.Sasa tunawambia tumekomboa goli, kama walitufunga goli moja, tumekomboa manne," alisema Rajabu.

Ameongeza ifikapo mwakani wakati wa kukaribia uchaguzi wa serikali za mitaa CCM mkoani Tanga haitafanya mzaha kuhakikisha wapinzani wanashindwa katika nafasi mbalimbali za uchaguzi.

Ameongeza mkoa huo umejipanga kuhakikisha kwanza inaongoza kitaifa katika kumpa kura nyingi Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za urais,  pia wanashinda kata zote 245, vijiji, vitongoji na Mitaa yote mkoani Tanga.

"Tanga tumejipanga kumpa kura nyingi sana Mheshimiwa Rais na tutaongoza kwa kura zote kuliko mkoa mwingine wowote lakini pia niwahakikishie kwamba kata zote 245, Vijiji, Vitongoji na Mitaa yote itakuwa ni CCM tunataka mkoa wetu uendelee kuwa wa kijani," Alisema.

Ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza watendaji wahakikishe wanazitendea haki fedha za miradi zinazoletwa na Rais kwamba zinatumika vizuri ili kuleta thamani halisi ya miradi husika.

Amewatoa wasiwasi wananchi wa Muheza kuwa mbunge wao MwanaFA amekuwa akijitahidi kuhakikisha analeta miradi ya naendeleo hivyo wasimuangushe.

Mkutano huo ambao pia ulitumika kumuaga aliyekuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Suleima Mzee ambaye aliwashukuru wana-CCM kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote Cha utumishi wake.


Mbunge wa Muheza na Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma maarufu MwanaFA akisalimiana na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga Ustadh Rajabu Abrahamani



Share To:

Post A Comment: