Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Victoria Mwanziva ameitaka Ofisi ya Mkurugenzi kupitia wataalam wa afya kuhakikisha kuwa wanavitunza na kuvilinda vifaa tiba vilivyopo katika zahanati na vituo vya afya ili viweze kusaidia wananchi katika kutoa huduma kwa muda mrefu zaidi.
Mwanziva ameyasema hayo akiwa katika kata ya Mundindi kwenye hafla ya uzinduzi wa zahanati ya kitongoji cha Chimbo iliyopo katika Kijiji cha amani kata ya Mundindi ambayo ujenzi wake umegharimu kiasi cha zaidi ya sh. Mil 74 huku serikali kuu ikitoa Ruzuku ya Sh. Mil. 50,000,000 sambamba na hafla ya kupokea vifaa Tiba vya kituo cha afya Mundindi vyenye thamani ya jumla ya sh. Mil. 150.
Aidha mkuu huyo wa Wilaya ameyaomba mashirika mbalimbali pamoja na wadau wa afya kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya kwa kuleta vifaa tiba ili wananchi waweze kupata huduma iliyo bora zaidi huku akiwataka wananchi hao kujiunga na mfuko wa bima ya afya ili waweze kupata huduma kwa gharama nafuu.
"Tunamshukuru mama yetu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa ni Rais ambaye anafika kusiko fikika, ametuletea sh. Mil. 200 kwaajili ya kukamilisha zahanati hii ya Kitongoji cha Chimbo, zahanati ya Mkiu, Kimelembe ambazo tayari zimekamilika na kuanza kutoa huduma pamoja na zahanati ya kijiji cha Ndowa ambayo ujenzi wake unaendelea na si hizo tuu bali hata katika miradi mingine kama ya elimu na barabara", Amesema Bi. Mwanziva.
Hata hivyo kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Sunday Deogratius amesema amepokea maelekezo hayo huku akiwapongeza wananchi kwa kujitoa kuanzisha ujenzi miradi mbalimbali ya maendeleo zikiwemo zahanati na vituo vya afya huku akiwataka kuendeleza jitihada hizo za kujitoa katika maendeleo ambapo serikali itawaunga mkono badala ya kukaa na kusubiri serikali ianzishe miradi hiyo.
Ameongeza kuwa serikali ya awamu ya sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua juhudi za wananchi kupitia mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga huku akiwataarifu kuhusu ujio wa fedha za Ruzuku ya maendeleo ya halmashauri ya Wilaya hiyo kiasi cha zaidi ya sh. Bil. 1.5 hivyo ameahidi kutenga kiasi cha Sh. Mil. 150 kwaajili ya ununuzi wa vifaa vingine zaidi katika kituo cha afya Mundindi.
"Ndugu zangu ujio wa fedha hizi za maendeleo, upatikanaji wa vifaa tiba na fedha za umaliziaji miradi ya ujenzi zinakuja kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na mbunge wetu Joseph Kamonga ambaye tumekuwa tukifanya nae kazi bega kwa bega na amekuwa akizunguka katika wizara mbalimbali ili kuona namna ya kupata fedha za maendeleo ya jimboni kwake lakini tunashukuru Rais wetu Dkt. Samia amekuwa akiona jitihada zetu na mbunge huyo matokeo yake amekuwa akiidhinisha fedha kwa kipindi kifupi tuu baada ya kuombwa". Amesema Mkurugenzi Ludewa.
Nao wananchi wamefurahishwa na utendaji mzuri wa kazi wa serikali pamoja na mbunge na diwani wao hivyo wameahidi kushirikiana kwa karibu na serikali katika kukuza maendeleo ya kata zao na wilaya kwa ujumla.
Post A Comment: