Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mh.George Simbachawene ametoa rai kwa Taasisi za Umma kuacha kununua na kutumia mifumo ya TEHAMA kutoka nje ya nchi na badala yake kuanza kutumia mifumo inayotengenezwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).

Akizunguza na Menejimenti na Watumishi wa eGA pamoja na Wanafunzi 100 kutoka vyuo mbalimbali nchini waliopo katika program maalum katika kituo cha Utafiti na Ubunifu cha Mamlaka kilichopo katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) jijini Dodoma,Waziri Simbachawene amesema wakati umefika kwa Taasisi na Serikali kwa ujumla kuanza kutegemea mifumo inayotengenezwa na wataalam wa ndani waliopo chini ya eGA.

Waziri Simbachawene amesema kwa sasa eGA tayari ina mifumo mbalimbali inayorahisisha utendaji kazi wa Taasisi na Idara za Serikali hivyo ni muhimu mifumo hiyo kutumika ili kuongeza ufanisi.

“Ipo baadhi ya mifumo ambayo tunajivunia hadi sasa inatokana na shughuli za ubunifu na utafiti zilizofanywa na vijana wetu kutoka katika kituo chetu hiki kwa weledi na utalaamu mkubwa, kazi ambazo hapo awali zilikuwa lazima zifanywe na wataalamu kutoka nje ya nchi.

Mfano Mfumo wa e-Mrejesho, Mfumo wa e-Mikutano, Mfumo wa Oxygen, Mfumo wa e-Board na e-Mrejesho ambao unasaidia sana wananchi kuwasiliana na Serikali”. Amesema Simbachawene.

Akizungumzia kituo hicho cha Utafiti na Ubunifu, Waziri Simbachawene amesema kuwa sasa Tanzania ipo kwenye Dunia ya Uchumi wa Kidijitali ambapo TEHAMA ni nyenzo muhimu hivyo Serikali imewekeza na kuweka kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA kwa kujenga miundombinu na mifumo inayosaidia kuboresha ufanisi wa uendeshaji shughuli zake lakini pia kutoa huduma kwa Umma


“Wizara kupitia eGA inasimamia na kukiboresha Kituo hiki ili kifanye tafiti mbalimbali hasa kwenye teknolojia mpya kama matumizi ya ‘Blockchain technologies’, Machine Learning, Artificial Intelligence na Internet of Things (IoT) ili na sisi tusibaki nyuma kama Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza” ameongeza Simbachawene.

Pia Mh.Simbachawene amewataka wanafunzi hao waliochaguliwa kushiriki program hiyo maalumu inayoendeshwa na kituo hicho kutumia ujuzi na uzoefu wanaoupata uwasaidie katika soko la ajira ikiwemo kujiajiri na kutengeneza ajira kwa vijana wenzao.

“Nafasi hii mliyopata ni muhimu sana kwenu nyie lakini kwa manufaa ya taifa letu hivyo itumieni kujifunza na kupata ujuzi utakaosaidia taifa na uchumi wetu” ameeleza Waziri Simbachawene.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Malamka ya Serikali Mtandao Mhandisi Benedict Ndomba ameongeza kuwa kupitia ubunifu, utafiti na mazoezi katika eneo la TEHAMA inawezesha nchi kushindana katika uchumi wa kidijitali kimataifa.

“Kuna mifumo mikubwa na shirikishi ambayo imetoka katika kituo hiki ikiwemo mfumo wa e-Mrejesho ambao tayari umetambuliwa na Benki ya Dunia kama mfumo bora unaotoa ushirikishaji kwa wananchi”. Amefanunua Mhandisi Ndomba.

Mhandisi.Ndomba ameongeza kuwa Mamlaka ya Serikali Mtandao tayari imeshanunua eneo la ekari nane (8) katika eneo la Kikombo jijini Dodoma kwa ajili kujenga kituo kikubwa zaidi kwa ajili ya kupanua shughuli za Ubunifu na Utafiti katika sekta ya TEHAMA.

Share To:

Post A Comment: