Kijana wa itifaki wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Iramba, John Samwel akimvika skafu Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa baada ya kuwasili wilayani Iramba kwenye hafla ya ya kumkabidhi Mkandarasi Henan Highway Engineering Group Ltd ya nchini China mradi wa ujenzi wa barabara ya Singida, Sepuka, Ndago hadi Kizaga katika hafla iliyofanyika Septemba 9, 2023 wilayani humo mkoani Singida.
................................................
Na Dotto Mwaibale, Iramba
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewataka wananchi watakaopitiwa na
mradi wa ujenzi wa barabara ya Sabasaba-Sepuka-Ndago-Kizaga mkoani Singida
yenye kilometa 77.6 kutojihusisha na hujuma yoyote
ikiwamo wizi wa vifaa ili ujenzi huo
ukamilike kwa thamani iliyopangwa.
Bashungwa aliyasema hayo Septemba 9,2023 katika hafla ya kumkabidhi
Mkandarasi Henan Highway Engineering
Group Ltd ya nchini China kuanza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango
cha lami.
'' Serikali imetoa fedha nyingi za utekelezaji wa miradi mbalimbali kote
nchini ikiwemo ya Mkoa wa Singida niwapongeze wananchi kwa ushirikiano mnaowapa
wakandarasi hata hivyo nitoe tahadhari ya wizi wa mali na vifaa vitakavyotumika
katika ujenzi naomba viongozi muwasisitize wananchi wanaozunguka maeneo ya
mradi kuepukana na uhalifu wa aina yoyote wa vifaa hivyo badala yake wavilinde
jambo litakalosaidia kulinda thamani halisi ya mradi huu na kukamilika kwa
wakati na ubora unaokubalika,'' alisema Bashungwa.
Katika hatua nyingine Bashungwa amewataka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kuhakikisha
wanamsimamia kikamilifu mkandarasi huyo na kukamilisha kazi hiyo kwa wakati
uliopangwa na ubora.
" Tanroads nyie ndio wenye dhamana ya kusimamia ujenzi wa barabara
hapa nchini jipangeni vizuri ujenzi
ukamilike ndani ya muda uliokusudiwa na kwa ubora na si vinginevyo",
alisema Bashungwa.
Bashungwa alisema ujenzi wa barabara hiyo utagharimu Sh.Bilioni 88.583 bila
kujumlisha kodi ya ongezeko la thamani VAT Sh.Bilioni 15.944 chini ya kampuni
hiyo.
Bashungwa alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta na watendaji wenzake pamoja na viongozi wote wa Mkoa wa Singida kwa kuandaa vizuri
hafla hiyo na kueleza kuwa Singida imefungua njia na sasa ataanza ziara ya
kwenda kuwakabidhi wakandarasi miradi iliyopo katika wilaya mbalimbali
akiambatana na wabunge wa maeneo ilipo ambayo imekwisha
tengewa fedha na Serikali.
Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba
Magharibi ambaye alikuwa mwenyeji wa makabidhiano hayo ya barabara hiyo pamoja
na Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu, aliwataka watanzania kuwa
wamoja hasa katika suala la kuinua uchumi wa nchi kazi ambayo Serikali ya Chama
Cha Mapinduzi CCM imeianza kwa kushirikisha sekta binafsi katika uwekezaji wa
uchumi.
'' Mimi kitaaluma ni mchumi hakuna nchi yoyote duniani ambayo inaweza
kukuza uchumi wake pasipo kuwekeza kwenye sekta binafsi na katika jambo hili
hatutarudi nyuma kwani litaongeza mapato ya nchi na kutuwezesha kutoa ajira
nyingi, ikiwa ni pamoja na za wauguzi
ambao watakuwa wakifanya kazi kwenye vituo vya afya tulivyo
vijenga nchi nzima,'' alisema Mwigulu.
Alisema kumekuwa na tofauti katika jambo hilo la uwekezaji hadi kufikia
hatua ya kutaka kufarakana kati yao ambao wanaamini kupitia uwekezaji watapiga
hatua na wenzao ambao hawautaki wakidai Serikali inaweza kufanyakazi hiyo peke
yake.
Mwigulu alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa
fedha za ujenzi wa barabara hiyo ambayo alikuwa ameanza kuiomba tangu alipoingia
bungeni kwa mara ya kwanza ambayo inakwenda kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya
za Ikungi, Iramba, Mkoa wa Singida na nchi kwa ujumla kutokana na kupata masoko
ya mazao yao..
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu licha ya kumshukuru
Rais Samia kwa kutoa fedha za ujenzi wa barabara hiyo alitoa onyo kwa
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe aache
kumsakama Rais Samia kwa kumteua Mohamed Mchengerwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI si kwa sababu ni mkwe
wake bali inatokana na uchapakazi wake uliotukuka kabla hajawa waziri na baada
ya kuwa Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na , Wizara ya Maliasili na Utalii .
Akitoa taarifa fupi ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed
Besta, alisema barabara hiyo inapita katika maeneo yenye uchumi wa kilimo,
misitu, madini na rasilimali nyingi ambazo hazichangii kikamilifu kwenye pato
la taifa kutokana na kutopitika kiurahisi.
‘’ Serikali inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha maeneo yote ya
kimkakati wa kiuchumi yanafikiwa kwa kuboresha barabara,’’ alisema Besta.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akitoa taarifa fupi ya maendeleo
ya mkoa huo alisema una vijiji 441 kati ya vijiji hivyo vijiji 341 tayari vina
umeme na vijiji 100 ambavyo havina wakandarasi wapo kazini.
‘’ Hapa Iramba wana vijiji 70 na vijiji ambavyo havina umeme ni vitano tu
na hadi kufika mwaka kesho vijiji vyetu vyote vitakuwa na umeme,’’ alisema
Serukamba.
Alisema mambo hayo yote yanafanyika kwa ufundi na ustadi wa Rais Samia
Suluhu Hassan ambaye amefanya mambo mengi katika miradi ya maji, sekta ya elimu
na mingine mingi ikiwemo minara ya simu na kilimo cha mazao yote alizeti,
mpunga, mahindi, dengu, vitunguu, pamba na kueleza kuwa anaamini sasa kuwa Mkoa wa Singida unakwenda kuwa kinara wa
uzalishaji wa mafuta ya kula na mazao yote ya chakula na biashara yanayolimwa mkoani hapa..
Mkurugenzi wa kampuni hiyo ilipewa kazi ya kujenga barabara hiyo,
Huang Lele alisema wamejipanga kukamilisha kazi hiyo kwa wakati uliopangwa na
akaomba kupewa ushirikiano kwa kuzingatia kuwa China na Tanzania ni marafiki wa
muda mrefu.
Katika mkutano huo Kamati ya maandalizi ya Kongamano la Shujaa wa Maendeleo
na Ustawi wa Jamii Tanzania SMAUJATA ambalo litafanyika Oktoba 7, 2023 ilitoa zawadi za fulana zenye
nembo ya upingaji wa ukatili kwa mgeni rasmi wa hafla hiyo Waziri wa Ujenzi,
Innocent Bashungwa na viongozi wengine mbalimbali waliokuwepo meza kuu zikiwa
na ujumbe usemao Kataa Ukatili wewe ni Shujaa.
Mkutano huo ulinogeshwa na mandhari nzuri na majukwaa makubwa ya kisasa yaliyopangwa viti kwa ustadi wa hali ya juu na kupambwa na wafanyakazi wabobezi katika masuala ya uwekaji wa majukwaa na upambaji hapa nchini kwenye mikutano na matamasha na Kampuni ya Montage Ltd inayofanya kazi zake katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani yenye makao yake makuu jijini Dar es Salaam ambapo kwa mawasiliano nao unaweza kupiga simu namba 0754999010 au 0657185580.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, akimtambulisha kwa wananchi na kumkabidhi ujenzi wa mradi huo Mkurugenzi wa kampuni hiyo ilipewa kazi ya kujenga barabara hiyo, Huang Lele.
Post A Comment: