Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula amewataka askari wa Jeshi la Uhifadhi kulinda maeneo yote yaliyohifadhiwa ikiwemo Misitu ya Asili ya mikoko, magofu katika visiwa vya Kilwa Kisiwani na Songomnara kwa weledi lakini pia kuwa na wivu nayo.
Mhe. Kitandula ameyasema hayo wilayani Kilwa kwenye ziara yake ya kwanza toka ateuliwe na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii.
Mhe. Kitandula yupo kwenye ziara ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambazo ni Wakala wa Huduma za Misitu kanda ya kusini, Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori(TAWA).
Aidha, Katika ziara hiyo Mhe. Kitandula alipata wasaa wa kutembelea mji wa Kilwa kisiwani ambao ni moja ya vituo vya Urithi wa Dunia unao tambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni.
Akitoa taarifa ya wilaya kuhusiana na shughuli za uhifadhi Mkuu wa Wilaya wa Kilwa, Mhe. Christopher Ngubuiagai alibainisha `changamoto ya uvamizi na Kuharibiwa kwa maeneo ya Kilwa Kisiwani pamoja na Songomnara ambayo ni Urithi wa Dunia kuwa yanatakiwa yapimwe na kuhifadhiwa vyema na kuwa vivutio vya utalii ambavyo vinatunzwa vyema.
“Kwani kuna wananchi wanayavamia na kung’oa Milango, madirisha kuharibu Matumbawe yaliyotumika kujengea majengo yale na wengine kujimilikisha kabisa hasa kwa magofu yaliko kwenye Mji Mdogo wa KIlwa Kivinje” aliongeza Ngubuigai.
Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa wakala wa Huduma za Misitu Kamishina Msaidizi kanda ya Kusini Bi. Manyisye Mpokigwa alisema kuwa Kanda ya Kusini imetenga maeneo muhimu katika wilaya tano (5) yani Kilwa, Nanyumbu, Tunduru, Songea na Nyasa na kufanya kuwa “beekeeping zones” kutokana na kuonekana kuwa na uzalishaji wa juu wa mazao ya nyuki ukilinganisha na maeneo yalioachwa.
“Kwa sasa Kilwa ndio wilaya pekee inayozalisha mazao ya nyuki ikiwemo asali na nta kutoka kwenye misitu ya jamii ya Mikoko” aliongeza Bi. Mpokigwa.
Naye Kamishina Msaidizi mwandamizi wa Uhifadhi, Abraham Jullu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA) akiwasilisha taarifa ya utendaji alisema kuwa TAWA inampango wa kuanzisha kifurushi kipya cha utalii kwa kuunganisha miji ya Kilwa na Selous ili mgeni apate ladha ya utalii wa fukwe, utalii wa magofu pamoja na utalii wa kuona Wanyamapori.
Post A Comment: