Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amewataka Watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kumpa ushirikiano wa kutosha katika utendaji kazi ili kufikia malengo yaliyowekwa huku akiahidi kutekeleza mipango yote ya kukuza utalii iliyowekwa na Waziri aliyepita ( Mtangulizi wake )
Ameyasema hayo leo wakati wa mapokezi yake akiwa ameambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Dunstan Kitandula katika Ofisi za Mtumba jijini Dodoma.
Mhe. Kairuki ameupongeza uongozi wa Wizara uliopita chini ya Waziri Mohamed Mchengerwa kwa kuchaguliwa katika nafasi ya Makamu wa Rais kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Utalii Duniani ( UNWTO) pamoja na kuchaguliwa kuwa katika Kamati Tendaji ya Utithi wa Dunia ( World Heritage)
Aidha, ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa aliyonayo kwake na kuahidi kutimiza wajibu wake kwa weledi na uadilifu mkubwa.
Naye, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula ameomba ushirikiano kwa Menejimenti ya Wizara ili kufikia matarajio ya Rais na pia amempongeza Waziri Mchengerwa kwa kuiacha Wizara kwenye mazingira mazuri.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa aliyoyafanya kwenye Wizara hiyo kwa kipindi cha miezi sita na kuwakaribisha Waziri pamoja na Naibu Waziri huku akiahidi kufanya nao kazi kwa umoja.
Post A Comment: